HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 16, 2021

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AWATAKA WATENDAJI KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

  

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe Othman Masoud Othman, akizungumza na watendaji wa ofisi yake juu ya utekelezaji wa majukumu ya kazi zao.

 


Na Raya Hamad – OMKR

 

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, amewahimiza watendaji wa Ofisi yake kuwa na mashirikiano ya pamoja katika kutekeleza majukumu ya kazi zao ili kuwe na ufanisi mzuri wa kazi wanazozifanya

Mhe Othman ameeleza hayo alipokutana na watendaji wakuu na wakuu wa vitengo na divisheni wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi  na Idara ya Mipango  Sera na Utafiti na kuwataka kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ili kuwe na msimamo na maamuzi ya pamoja kwa kila hatua

Aidha Mhe Masoud amewakumbusha  watendaji wa Ofisi  kuwa wabunifu ili watakapoondoka waache kumbukumbu nzuri  kwa Taasisi na wanaowaogoza  pamoja na kufahamu kuwa kazi yeyote inahitaji kujitolea ili kuyafikia mazuri, kuwa tofauti kwa kutokukata tamaa kulingana na rasilimali zilizopo

Amefahamisha kuwa katika kuongoza wafanyakazi kiongozi lazima afahamu sheria za utumishi mfanyakazi anapofanya vizuri kumzawadia na kuwapa heshima yao kwani haki na wajibu ni mambo yanayokwenda sambamba hasa katika utendaji

Viongozi wanatakiwa kusimamia sheria na taratibu hivyo Wafanyakazi wapewe heshima yao,  kusimamiwa haki zao ,  wajibu wao wa kufanyakazi na kupewa  maslahi yao ambayo wanastahiki jambo ambalo  limeondoka  katika utamaduni wa kufanya kazi  

‘Imeshakuwa ni mazowea na tabia ya kuwafanya watumishi wa Serikali ni watumwa wa Serikali ni muhimu haki ifuatane na wajibu hata kama ni kidogo’ alisisitiza Makamu wa Kwanza wa Rais

Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Masoud Othman Masoud amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa majukumu ya Ofisi yake na taasisi zilizo chini yake ili wafahamu yale yanayotekelezwa  kwa  kuonesha sura ya halisi ya Ofisi  

Kuhusu suala la kiutendaji  amewaagiza viongozi kuona  kila mfanyakazi  anawajibika  na kufahamu majukumu yake ya msingi kwani mabadiliko hayawezi  kutokea  bila ya  kuwepo uwajibikaji na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea  bali waendane na kasi ya mabadiliko ya utendaji

‘mfanyakazi usisubiri kuulizwa jambo hili la kiutendaji limefikia wapi? wakati unafahamu kuwa ili kazi ziendelee ni wajibu wako kutekeleza majukumu yako pamoja na kuwa mbunifu  katika kazi zenu’

Katibu Mkuu Bi Khadija Khamis Rajab ameomba watendaji na wakuu wa vitengo kuhakikisha maelezo yaliyotolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Othman Masoud Othman kuwa yanazingatiwa na yanafanyiwa kazi kwa kila mmoja kufahamu masuala ya msingi kwa lengo la kuleta ufanisi .

Aidha  ameahidi kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itaendelea kuweka mazingira mazuri ya Ofisi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa ikiwa ni kufanya kazi kwa bidii kuwajibika, kufuata sheria na taratibu na kuzawadia wafanyakazi pale panapostahiki.

Nao Wakurugenzi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wameahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo katika kushughulikia masuala yao ya kiutendaji pamoja na  kuhakikisha wanasimamia vyema maslahi ya watumishi , kufikisha huduma kwa wananchi wanaowahudumia na kuunganisha taratibu  za uratibu za sera na utafiti  

Mhe Makamu wa Kwanza wa Rais amekamilisha ziara yake kwa Unguja na Pemba kwa   kuzipitia Taasisi zilizochini yake na kumalizia Ofisi Kuu Unguja kuzungumza na watendaji wakuu na wakuu wa vitengo wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi, Idara ya Mipango Sera na Utafiti katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisini kwake Migombani

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ina jukumu la kuratibu mambo yote yanayohusu Ofisi ya Faragha na Makamu wa Kwanza wa Rais, Kuratibu masuala ya Uendeshaji na Mipago ya Ofisi, Kuratibu masuala ya Watu wenye Ulemavu, Kusimamia masuala ya Mazingira, Kuratibu na kusimamia masuala ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, Kuratibu masuala ya Udhibiti wa Dawaza Kulevya.

No comments:

Post a Comment

Pages