HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 18, 2021

TUTAENDELEA KUBORESHA SERA NA SHERIA YA UVUVI-ULEGA



 

 

 

 

 

 

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.

 

Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

 

Serikali imesema ipo tayari kuendelea kupitia Sera na Sheria ya Uvuvi nchini ili iweze kukidhi mahitaji ya wavuvi wadogo kama ambavyo imekuwa ikifanya hivyo mara kwa mara pale inapohitajika.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum kutoka mkoani Kagera Mhe. Neema Lugangira ambaye alitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuhakikisha Sera na Sheria ya uvuvi nchini inakidhi mahitaji ya wavuvi wadogo.

Mhe. Ulega amesema kuwa katika kuhakikisha wavuvi wadogo nao wananufaika na Sera na sheria iliyopo, Wizara ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 2015 ambayo imezingatia mahitaji ya wadau wote wa sekta ya uvuvi na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi nchini.

“Aidha Wizara ilifanya mapitio ya sheria namba 6 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania ya mwaka 1980 na kutunga sheria namba 11 ya mwaka 2016 ili kuimarisha shughuli za utafiti nchini” Aliongeza Mhe. Ulega.

Mhe. Ulega ameongezea kuwa mwaka 2020 Wizara ilifanya marekebisho madogo kwenye sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 kwa lengo la kuimarisha shughuli za ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za Uvuvi nchini.

“Mhe. Spika Wizara inaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 ili iweze kuendana na mahitaji halisi ya sasa ya kisekta ikiwemo kutatua kero mbalimbali za wadau wa sekta ya uvuvi hususani wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji” Alisema Mhe. Ulega.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Lugangira ambaye alitaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuhakikisha wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi wananufaika ipasavyo baada ya kuuza samaki na mabondo kwa pamoja, Mhe. Ulega mbali na kukiri kuwa mabondo yana thamani kubwa hivi sasa hasa kwenye masoko ya bara la Asia, amesema  kuwa Sheria ya Uvuvi na kanuni zilizopo hivi sasa zinayatambua mabondo kama moja ya bidhaa zinazotokana na samaki hivyo aliahidi kupokea rai na ushauri uliotolewa na Mhe. Lugangira na kwenda kuufanyia kazi.

Mhe. Ulega alihitimisha majibu yake kwa kujibu swali la nyongeza la Mhe. Lugangira aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kuwalinda wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi dhidi ya ukatili wanaofanyiwa wakati wa utekelezaji wa shughuli zao ambapo amesema kuwa Serikali ilifanya maboresho ya Sera ya Uvuvi ya mwaka 2015 na kuweka jukwaa maalum la kuwasaidia wanawake ikiwa ni pamoja na kuwatambua moja kwa moja wanawake wafanyabiashara wa samaki.

No comments:

Post a Comment

Pages