Baadhi ya washiriki wa semina ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB.
Dar es Salaam, 17 Machi 2020 - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Uwekezaji Geoffrey Mwambe amewataka Watanzania kuiunga mkono Benki ya
CRDB kwa kwa kupata huduma katika benki ili kuendelea kuiimarisha kwani
benki hiyo inaonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kuwainua wananchi
kiuchumi. Waziri Mwambe amezungumza hayo wakati wa Semina ya Uwekezaji
na Fedha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB na kufanyika katika Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere na kuhudhuriwa na watu zaidi
ya 3,000 ambapo wengi wao walihidhuria kupitia mtandao.
“Benki hii imekuwa ikiwathamini sana Watanzania kwa kuandaa kuanzisha
huduma na programu wezeshi kiuchumi kwa wananchi. Hivyo tunapaswa
kuiunga mkono ili iendelee kuwepo na kuwahudumia Watanzania. Fungueni
akaunti katika Benki hii na mtumie huduma za kisasa za kidijitali ambazo
zinatolewa hapa,” alisistiza Waziri Mwambe.
Waziri Mwambe alisema kwa kuwa Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele
katika kusaidia agenda za maendeleo ya nchi anaialika Benki hiyo
kushiriki katika mkakati wa kupanua wigo wa uwekezaji nchini kwa
kuanzisha dirisha maalum la viwanda ili kuchochea kuimarika viwanda
vidogo na vikubwa kwa kuwawezesha wawekezaji kupata mitaji ya uhakika.
“Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hii Abdulmajid Nsekela ndio
Mweneyeki wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) nimuombe ashawishi na
mabenki mengine kutekeleza hili ili. Nitaandaa mkutano na umoja huu
iliyuweze kulijadili hili kwa upana,” aliongezea Waziri Mwambe.
Aidha, Waziri Mwambe alisema alibainisha kuwa ili sekta binafsi iweze
kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kunatakiwa kutengenezwa
mazingira mazuri ya kuwawezesha watu na makampuni kupata fedha za
kuwekeza. Alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha
mazingira ya biashara kwa kuondoa urasimu na kupunguza utitiri wa kodi
na tozo ili kupunguza gharama za uwekezaji nchini ikiwa ni utekelezaji
wa agizo la Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
“Mkurugenzi Mtendaji naomba nikuhakikishie mkiweza kuwawezesha
wawekezaji hawa kuwekeza katika viwanda faida ni kubwa mno katika uchumi
wa taifa letu. Tutaweza kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa, ajira
zitakuwa za kutosha, mzunguuko wa fedha utaongezeka, na hata faida
mtakayopata itakuwa zaidi ya hii shilingi bilioni 165 ambayo mmeipata
mwaka jana,” alisema Waziri Mwambe.
Katika hotuba yake Waziri Mwambe aliainisha kuwa mpango wa Serikali
nikuachana na kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa kutengeneza bidhaa
hapa nchini kupitia viwanda vya ndani na kuzitafitia soko nje ya nchi.
“Mfano kwa upande wa zao la pamba tumeweka mkakati ndani ya miaka mitatu
hatutaki kuona tuna uza pamba ghafi nje,” amesema Waziri Mwambe.
Waziri Mwambe ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa Semina hiyo ya
Uwekezaji na Fedha huku akiwataka wananchi kujenga utamaduni wa
kujiwekea akiba na kuwekeza katika masoko ya mitaji ili kujijenga
kiuchumi.
“Niwahamasishe kwa kuanza kuwekeza ndani ya Benki yetu ya CRDB. Tukiwa
tunaweka akiba na kutazama riba, tukumbuke pia kuna gawio, ambalo
linafaida kubwa. Sasa hivi Benki hii tunaimiliki kwa 80%, tuwekeze
tufike 100%,” aliongezea huku akisisitoza juu umuhimu wa kufikisha elimu
hiyo hadi vijijini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid
Nsekela alisema malengo ya Semina hiyo ni kuona Watanzania wengi zaidi
wanashiriki katika fursa za uwekezaji hapa nchini pamoja na kupata
uelewa wa huduma za benki hiyo zitakazowasidia kuwa wawekezaji wazuri.
Akielezea kuhusu program mbalimbali za elimu ya fedha na uwekezaji kwa
umma, Nsekela amesema Benki ya CRDB ikiwa benki ya kizalendo inajivunia
kwa kuwa mstari wa mbele katika kufikisha elimu ya fedha na uwekezaji
kwa Watanzania. Nsekela pia alimhakikishia Waziri Mwambe kuwa Benki hiyo
itaendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi ili kujenga uwajibikaji wa
kifedha katika jamii na kuongeza ujumuishi wa kifedha.
“Watanzania wengi wamekuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha kwasababu
hawana elimu ya kutosha hivyo kupelekea wengi kuogopa. Lakini kupitia
elimu hii tunaamini wengi sasa wataweza kujiunga na taasisi za kifedha
lakini pia kichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hii
pamoja na masoko ya mitaji,” alisema Nsekela.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alimshukuru
Waziri Mwambe kwa kuikaribisha benki hiyo kushirikiana na Serikali
katika kutekeleza mikakati ya kuchochea uwekezaji nchini, ambapo
alimhakikishia kuwa benki hiyo itakwenda kuandaa sera ambayo itakwenda
kuelekeza na kusimamia uwezeshaji katika sekta ya viwanda na kuwa
pendekezo la kuanzisha dirisha la viwanda limepokelewa kwa ajili ya
utekelezaji.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika Semina hiyo ya Uwekezaji na fedha
ikiwamo; Biashara ya Hisa Kidijitali iliyowasilishwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa, Mada ya
Uwekezaji wa Pamoja iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji UTT
AMIS, Daniel Mbaga, Mada ya Gawio kwa Wanahisa iliyowasilishwa na Katibu
wa Benki ya CRDB, John Rugambo, Mada ya Uwekezaji Endelevu wa Mali
iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Joachiam and Jacob Attorneys, Waki
Grace Joachim, Mada ya Uwekezaji kupitia Huduma na Bidhaa za Benki na
Bidhaa iliyowasilishwa na Meneja wa Idara ya Hiiazina Benki ya CRDB,
Hemed Masumai, na Mada juu ya Huduma za Benki ya CRDB Kufanikisha
Uwekezaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa
Benki ya CRDB, Boma Raballa.
Washiriki wa Semina hiyo waliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina
hiyo huku wakisema imesaidia sana kuongeza uelewa juu ya masuala ya
uwekezaji na huduma za kifedha. Baadhi ya washiriki walipendekeza semina
hiyo kufanyika hata mara tano kwa mwaka kwani bado uelewa wa masuala ya
uwekezaji katika jamii ni mdogo.
Akitoa shukrani kwaniaba ya washiriki, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick
Sumaye ambaye pia ni Mwanahisa wa Benki ya CRDB aliishuru Bodi na
Menejimenti ya benki hiyo kwa kuendelea kutekeleza programu za elimu ya
uwekezaji na fedha kwa Watanzania. Sumaye pia alitumia nafasi hiyo
kuwakaribisha Watanzania wengine kuwekeza katika Benki yao ya CRDB.
“Faida ya kuwekeza huku ni kubwa mno, niwakaribishe mjionee wenyewe,”
alisisitiza Sumaye
No comments:
Post a Comment