Kipa Derick Katto wa timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) akipatiwa matibabu baada ya kuumia katika mchezo wa soka dhidi ya Uchukuzi wa Michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Eulitery Mholiery, kipa wa Uchukuzi akijiandaa kudaka mpira wa penati iliyopigwa na Barnabas Mwashambwa wa timu ya Shirika la Maendeleo ya Petrol Nchini (TPDC), katika mchezo wa soka wa Kombe la michuano ya Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Timu ya kuvuta Kamba ya wanawake ya Uchukuzi ikiwavuta wenzao wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Timu ya kuvuta Kamba ya wanaume ya Uchukuzi ikiwavuta wenzao wa Ukaguzi kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Na Mwanndishi Wetu, Mwanza
TIMU za soka za Uchukuzi na Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC), leo zimetoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
TPDC walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa kwa njia ya penati na Barnabas Mwashambwa baada ya nahodha Dalush Shija kufanyiwa madhambi na Ramadhani Madebe wa Uchukuzi katika eneo la hatari.
Pamoja na mchezo huo kuwa mkali, na Uchukuzi kucheza pungufu baada ya Madebe kutolewa kwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili, waliweza kusawazisha kupitia kwa Rahim Ayeshi aliyeunganisha krosi safi ya Idrisa Bahatisha.
Hatahivyo, bado Uchukuzi inaongoza kundi B ikiwa na alama nne na magoli nane ya kufunga, huku TPDC wakishika nafasi ya pili nao wakiwa na alama nne na magoli saba ya kufunga. Timu ya Wizara ya Kilimo inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama tatu huku Jiji Mwanza na Wizara ya Mambo ya Nje zikiwa hazina pointi.
Katika michezo ya Kamba timu ya wanaume TPDC iliwavuta Kilimo kwa mivuto 2-0; wakati Tanesco wakishindwa kufurukuta mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa mivuto 2-0 na Uchukuzi wakiwavuta Ukaguzi kwa mivuto 2-0.
Katika michezo ya wanawake timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliwaadhibu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa mivuto 2-0; na Taasisi ya Saratani Ocean Road ilichapwa lna Uchukuzi kwa mivuto 2-0.
Michuano hiyo itaendelea leo katika michezo ya kuvuta Kamba wanaume Uchukuzi watakutana na MWAUWASA; huku Tanesco watacheza na Kilimo; na NCAA watapepetana na Jiji Mwanza; wakati kwa wanawake Tanesco itawakaribisha Wizara ya Mambo ya Nje; nayo Kilimo itakutana na MWAUWASA.
Katika michezo ya soka timu ya MWAUWASA watawakaribisha Tanesco; huku Wizara ya Mambo ya Nje itacheza na Jiji Mwanza; wakati katika netiboli timu ya Ikulu itacheza na Kilimo; Jiji Mwanza watakutana na TPDC na Wizara ya Mambo ya Ndani watacheza na MWAUWASA.
No comments:
Post a Comment