Meneja Mradi wa TTCS Charles Leonard akielezea mafanikio ya mradi huo kwa wanavijiji na halmashauri za vijiji na wilaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Matuli, Lucas Lemomo akieleza namna Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta
ya Mkaa (TTCS) ulivyomuwesha kutetea udiwani wake 2020.
NA SULEIMAN MSUYA
USIMAMIZI
Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) unaotekelezwa katika vijiji zaidi
ya 30 na wilaya tatu za mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa ni sababu kubwa
kwa waliokuwa madiwani kuchaguliwa mwaka 2020.
USMJ
mkoani Morogoro unatekelezwa katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na
Morogoro DC ambapo vijiji zaidi ya 30 vinanufaika kiuchumi, kijamii,
maendeleo na uhifadhi.
USMJ
katika vijiji hivyo inatekelezwa na Mradi wa Kuleta Mageuzi katika
Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) kupitia Shirika la Kuhifadhi Misitu ya
Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu
Tanzania (MJUMITA) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi
(SDC).
Ushuhuda huo
umetolewa na Madiwani Lucas Lemomo wa Kata ya Matuli wilayani Morogoro
na Hassan Kambenga Kata ya Kisanga wilayani Kilosa wakati wakizungumza
na mwandishi wa habari hii.
Diwani
Lemomo amesema Mradi wa TTCS ulifika kwenye kata katika awamu ya kwanza
ya udiwani wake mwaka 2015 ambapo vijiji vitatu vya Matuli, Diguzi na
Tununguo.
Lemomo ambaye
ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro amesema ujio wa mradi
ulihakikisha kunakuwepo na matumizi bora ya ardhi na kitambua mipaka ya
misitu ndio shughuli za uzalishaji zikaanza.
"Katika
kata ya Matuli, Tarafa ya Ngerengere, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), 2015/2020 imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kupitia TTCS.
Yote
ambayo tulikuwa tumeahidi wananchi, kwa mfano mimi niliahidi sekondari
ambapo awali tulijenga madarasa mawili kwa miaka 10 ila fedha za misitu
zimejengwa majengo mapya na shule umeanza," amesema.
Ilani
ya CCM katika Ibara ya 69 (F), Sera ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria
ya Misitu ya Mwaka 2002 kwa pamoja vinasisitiza umuhimu wa wananchi
wanaozungukwa na misitu kunufaika na rasilimali hiyo.
Lemomo
amesema pia wamejenga ofisi za vijiji za kisasa, wajumbe wa serikali ya
kijiji na wenyeviti wanapewa posho na wananchi wamekuwa na uchumi mzuri
hivyo kufanya shughuli za maendeleo.
Diwani
amesema wamefanikiwa kujenga Zahanati kwenye kijiji cha Lulongwe ila
wameishia njiani kutokana na vikwazo vya Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS)
"Niweke
wazi kuwa bila TTCS sisi madiwani ambao tunatoka kwenye vijiji vyenye
miradi hatungerudi kwani zaidi ya shilingi milioni 600 zimepatikana na
kutekeleza miradi huku serikali ikipeleka shilingi milioni 15," amesema.
Mwenyekiti
huyo wa halmashauri ameyataka mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali
kuendeleza miradi hiyo kwa vijiji ambavyo vina misitu ya asili.
Amesema
halmashauri ya Morogoro inatarajia kutenge fedha za kutekeleza mradi
kwenye vijiji viwili kwa kuwa manufaa ya vijiji vitano vya Matuli,
Diguzi, Lulongwe, Mlilingwa na Tununguo yameonekana.
Kuhusu
changamoto ya TFS Lemomo amesema ipo haja kwa serikali kuangalia huu
mfumo ili uwe endelevu na sio kukwamisha kama anavyodai.
Amesema
vijiji vyenye USMJ uhifadhi umeongezeka kwa asilimia kubwa huku
wanavijiji wakinufaika tofauti na vijiji visivyo na mradi.
Kwa upande Diwani Kambenga wa Kata ya Kisanga amesema TFCG imechochea maendeleo makubwa katika vijiji 20 vya wilaya Kilosa.
"Sisi
Kisanga tuna vijiji viwili ambavyo vimenufaika na mpango wa matumizi
bora ya ardhi, ujenzi wa ofisi za kijiji, madarasa yamejengwa, wananchi
wamelipiwa bima ya afya CHF.
Pia
ofisi ya kijiji imejengewa choo cha kisasa, elimu ya utawala bora na
uhifadhi zimetolewa hali ambayo kinawapa motisha wananchi kuilinda
misitu," amesema.
Amesema kupitia miradi hiyo hakutumia nguvu kubwa kujinadi kwani wananchi wameona matunda ya utawala wake.
Kambenga amesema Serikali inapaswa kutenga bajeti kila mwaka ili kuendeleza miradi hiyo kwa vijiji vipya.
Diwani
huyo amesema changamoto kubwa ni TFS kutowapa ushirikiano wavunaji wa
mazao ya misitu waliopo kwenye vijiji vya USMJ hali ambayo inakatisha
tamaa wanavijiji.
"Wavunaji
wa mazao ya misitu yasiyo na mpango wa matumizi bora ya ardhi wanapewa
huduma nzuri kuliko waliopo kwenye vijiji vya mradi," amesisitiza.
Akizungumzia mafanikio ya TTCS Meneja Mradi Charles Leonard amesema zaidi ya shilingi bilioni 3.5 zimepatikana hadi sasa.
Amesema
shilingi bilioni 2 zimeelekezwa kwenye Serikali za vijiji na kutekeleza
miradi ya maendeleo kama elimu, afya, maji na uhifadhi.
"Shilingi bilioni 1.5 wamepata wavunaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa na mbao huku wakizingatia uhifadhi," amesema.
Meneja huyo amesema iwapo misitu itatunzwa na kutumiwa kiundelevu inamchango mkubwa kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
Leonard ameiomba Serikali kuweka mkazo katika USMJ kwa kuwa ina matokeo chanya kwa asilimia 80.
No comments:
Post a Comment