Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Joackim Otaro (kulia) kwa niaba ya mkuu wa mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jumuiya za watumia maji wa Bwawa la Songwa na Nhumbu yaliyopo mkoani Shinyanga, akikabidhi pikipiki mbili kwa viongozi wa jumuiya hizo katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shinyanga hivi karibuni.
Viongozi wa Jumuiya ya watumia maji wa Bwawa la Nhumbu na Songwa wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi na viongozi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Kati.
Na Dotto Mwaibale, Shinyanga
WANANCHI mkoani Shinyanga wameombwa kutumia rasilimali za maji vizuri kwa kuwa ndio tegemeo katika ustawi wa kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Joackim Otaro kwa niaba ya mkuu wa mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jumuiya za watumia maji wa Bwawa la Songwa na Nhumbu yaliyopo mkoani humo.
"Ndugu zangu wana Shinyanga niwaombe tutumie rasilimali zetu za maji vizuri maana maji hayana mbadala, maji ni uhai na ndio tegemeo letu katika ustawi wa kiuchumi, kijamii na kimazingira." alisema Otaro.
Otaro alisema madhumuni ya kuzindua Jumuiya za Watumia maji wa Bwawa la Nhumbu na Bwawa la Songwa ambazo zimeundwa kwa ufadhili wa Bodi ya Maji ya Bonde la kati kwa sheria namba 11 ya mwaka 2009 na Sera ya maji ya mwaka 2002 ni kutunza vyanzo vya maji.
Alisema Jumuiya za watumia maji ni chombo cha chini katika ngazi ya jamii kinachoundwa kwa lengo la kuiwezesha na kuiunganisha jamii ya watumia maji wa chanzo husika kwa pamoja, ili kujadili changamoto zao na kuandaa mipango ya usimamizi na uhifadhi wa chanzo chao cha maji kwa lengo la kupunguza vitendo vya uchafuzi, uharibifu wa miundo mbinu, migogoro ya matumizi ya maji.
"Suala la usimamizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila mtu si jukumu la Serikali peke yake, hivyo linahitaji nguvu ya pamoja katika kupanga na kusimamia mipango mbalimbali ya kuendeleza uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji." alisema Otaro.
Aidha, Otaro aliongeza kuwa Bodi ya Bonde la Kati kama chombo chenye dhamana na Usimamizi wa Rasilimali kwenye eneo la bonde lake, waendelee kutoa hamasa, elimu na hata kuunda jumuiya za watumia maji kwenye maeneo mengine yenye changamoto za namna hiyo hususan katika mkoa huo wa Shinyanga na alieleza juhudi hizo walizozianzisha ziwe endelevu pamoja na kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatambuliwa, kuwekewa mipaka na kuhifadhiwa vizuri ili visiharibiwe na kuchafuliwa na shughuli zozote za kibinadamu.
Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Kati, William Mabula alisema kuna umuhimu mkubwa mno wa jumuiya hizo kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji.
Alisema tukisiliza sekta ya maji inavyojadiliwa katika ngazi ya kimataifa na hata ngazi za Serikali kumekuwa na msisitizo kwenye lile tone la maji linalotoka lakini si habari ya chanzo chake na jinsi yanavyohifadhiwa.
"Serikali imeendelea kuhimiza utunzaji wa vyanzo vya maji kama tulivyomsikia hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akihimiza utunzaji wa vyanzo hivyo kuanzia ngazi za chini na ndio kama hizi jumuiya tulizozianzisha." alisema Mabula.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi, Bodi ya Maji Bonde la Kati, Nelea Bundala, alisema mchakato wa uundaji wa jumuiya hizo mbili ulianza Septemba mwaka 2020 baada ya maagizo ya kamati ya Taifa ya ufungaji migodi ya kuitaka Bodi ya maji Bonde la Kati kutembelea mabwawa yote ya Williamson na kuangalia changamoto zilizopo zinazopelekea kuharibika kwa ubora wa maji na kupungua kwa wingi wa maji.
Alisema Bodi ilitekeleza agizo hilo na ilitembelea na kutathmini hali ya vyanzo hivyo na ilionekana kwamba kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa watumia maji wa mabwawa hayo yote, pamoja na kuwezesha kuunda chombo cha kijamii yaani Jumuiya za watumia maji kwa Mujibu wa sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 inavyoelekeza.
" Katika mchakato huo mikutano ilifanyika kila kijiji na wawakilishi wa kila kijiji walipewa mafunzo yatakayowawezesha kusimamia vyanzo hivyo vya maji vizuri." alisema Bundala.
Bundala alisema kwa Jumuiya ya Nhumbu vijiji vinavyohusika ni Mwamalili, Bushora, Songwa, Buchachi, Buganika, Mwigumbi, Seseko na Mpumbura na kwa Bwawa la Songwa jumuiya inahusisha vijiji vya Songwa, Buganika, Buchambi, Mwigumbi, Maganzo, Ikonongo na Masagala.
Aidha Bundala alisema kuwa wawakilishi hao walitengeneza katiba ambayo ndani yake kuna sheria ndogondogo ambazo zitatumika kuzuia uharibifu mbalimbali unaoendelea katika mabwawa hayo, ikiwemo kulima karibu na mabwawa, kunywesha mifugo kiholela bwawani, uvuvi haramu, uchenjuaji madini bwawani, kuosha vyombo, kufua ndani ya vyanzo vya maji.
Alisema mambo hayo yote yanayoharibu ubora na wingi wa maji na kuwa madhara ya uharibifu huo ni makubwa kwani kina cha maji kinapungua siku hadi siku na matokeo yake yanakua ni mafuriko.
Katika uzinduzi huo Bodi ya Maji Bonde la Kati ilitoa pikipiki mbili aina ya Yamaha, simu za mkononi, katiba na baadhi ya vifaa vya ofisini kwa ajili ya kusaidia jumuiya hizo katika kazi za kila siku za kutunza vyanzo vya maji.
No comments:
Post a Comment