HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 13, 2021

Jafo: Nunueni tumbaku iliyokaushwa kupitia mabani ya kisasa


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo akikagua mabani ya kisasa ya kuchomea tumbaku Wilayani Urambo, Tabora. Mabani hayo ya kisasa yanatumia kuni kidogo jambo ambalo linasaidia katika kupunguza uharibifu wa misitu.



NA LULU MUSSA, TABORA 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo ameagiza vyama vya msingi Mkoani Tabora kununua tumbaku iliyokaushwa kupitia mabani ya kisasa.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri Jafo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua mabani yanayotumika kukausha tumbaku Wilayani Urambo na kuwapongeza wakazi wa Wilaya hiyo kwa kutumia teknolojia ambayo inapunguza ukataji wa misitu kwa kiwango kikubwa.

“Natoa rai kwa vyama vyote vya msingi, kununua tumbaku ambayo imekaushwa kupitia mabani haya ya kisasa kwasababu viwango vyake vya ubora viko juu na ukaushaji wake unalinda mazingira yetu,” Jafo alisisitiza.

Awali akiwasilisha taarifa ya Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Urambo Christina Kangwa amesema, kwa sasa mabani hayo yamejengwa kwa wingi katika Wilaya yake na hamasa inaendelea kukahikisha inakuwa ni moja ya agenda ya kuwahimiza wananchi kubadili teknolojia ya zamani na kutumia teknojia Rafiki kwa mazingira.

“Azma ya Serikali ni kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa kupunguza ukataji misitu kwa wingi, Tumbaku ni zao kuu la Biashara Wilayani kwetu hivyo tunahakikisha maendeleo ya Viwanda yanaenda sambamba na hifadhi ya Mazingira,” Kangwa alisisitiza.

Mmoja wa wakulima wa Tumbaku Shija Ramadhani amesema kupitia ujenzi wa mabani hayo ya kisasa, tumbaku inayokaushwa ina soko kubwa pia ukaushwaji wake ni rahisi kwa kuwa hutumika vipande vidogo vya kuni na si magogo makubwa kama zamani.

Wakazi wa Wilaya ya Urambo wanajishughulisha zaidi na kilimo cha Tumbaku, kwasasa kaya nyingi zimebadili mfumo wa ukaushaji wa tumbaku kutoka ule wa awali wa kutumia magogo makubwa na sasa ujenzi wa mabani ya kisasa yamepunguza uharibifu wa mazingira kwa kuwa unatumia kuni kidogo.

No comments:

Post a Comment

Pages