kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto na ujenzi wa kituo cha mawasiliano Taasisi ya Saratani Ocean Road
Dar es Salaam, Tanzania
Benki ya CRDB imetangaza kusajiliwa kimataifa kwa mbio zake za hisani za “CRDB Bank Marathon” ambazo zilizinduliwa mwaka jana kwa kauli mbiu ya “Kasi Isambazayo Tabasamu,” zikilenga kuhamasisha kuchangia maendeleo na kusaidia wenye uhitaji katika jamii.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa CRDB Bank Marathon 2021, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa amesema mapema mwaka huu mbio hizo zilipewa usajili wa kimataifa na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AMIS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics)
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu mpya wa CRDB Bank Marathon 2021.
“Ninafuraha kuwajulisha kuwa mafanikio ambayo tuliyapata mwaka jana yamefungua milango kwa CRDB Bank Marathon kutambuliwa na kupata usajili wa kimataifa. Usajili huu wa kimataifa sio tu unakwenda kupanua wigo wa kusambaza tabasamu, lakini pia unafungua fursa za kibiashara kwa Watanzania kwani tunarajia wakimbiaji wengi wa kimataifa kujumuika nasi,” aliongezea Tully huku akibainisha kuwa usajili huo wa kimataifa pia utasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.
Akielezea kuhusiana na msimu wa CRDB Bank Marathon 2021, Tully alisema lengo la mwaka huu ni kukusanya shilingi milioni 500 kusaidia gharama za upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Alisema pamoja na kuendelea kusaidia eneo hilo, sehemu ya fedha itakayo kusanywa itapelekwa kusaidia ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja “Call Centre” kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla, akizungumza katika uzinduzi huo.
“Kama mnavyofahamu magonjwa ya saratani ni moja ya changamoto ambazo zinakiabili jamii yetu. Ili kupambana nayo na kupunguza tatizo tunahitaji kutoa elimu ya kutosha na kurahisisha utaratibu wa kukutana na madaktari na kupata huduma. Kituo hiki kitakwenda kurahisisha yote haya,” alisisitiza Tully.
Akizungumzia namna ya kushiriki mbio hizo ambazo zinatarajiwa kufanyika tarehe 15 Agosti 2021, Tully alisema dirisha la usajili kwa wakimbiaji litafunguliwa siku ya jumamosi ya tarehe 15 Mei 2021 ambapo watu binafsi au vikundi wataweza kusijajili kushiriki kupitia tovuti maalum ya mbio hizo ya www.crdbbankmarathon.co.tz .
Makamu wa Rais wa Chama cha Baiskeli Tanzania, Hussein Ali, akizungumzia namna watakavyoshitiki katika mbio hizo.
“Kujisali na kuchangia mbio hizi kwa binafsi ni shilingi 30,000 au kupitia vikundi ni 25,000. Malipo yanaweza kufanyika kupitia matawi ya Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App, mitandao ya simu na kupitia kadi ambazo zinawawezesha hadi watu wa nje ya nchi kufanya malipo,” alisema Tully huku akisisitiza kuwa fedha hizi zote zitaelekezwa katika kusaidia gharama za upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo na ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Aidha mkurugenzi huyo aliwahamasisha Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo huku akibainisha kuwa safari hii mbio hizo zinajumuisha km 42.2, km 21.1, km 10, km 5 na mbio za baiskeli za km 65.
No comments:
Post a Comment