Kiwanda cha kuzalisha vigae cha Goodwill Tanzania Ceramic Company Limited kimewakaribisha watanzania kutumia bidhaa zake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa kuwa bidhaa zake ni bora.
Akizungumza katika ziara ya waandaaji wa kipindi maalum kinachoangazia mchango wa madini ujenzi na madini ya viwanda kwenye Sekta ya Madini kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakiongozwa na Meneja Habari na Mawasiliano wa Tume ya Madini, Greyson Mwase, leo tarehe 10 Mei, 2021 Wilayani Mkuranga Mkoani Pwani, Meneja Rasilimaliwatu wa kiwanda hicho Jerry Marandu amesema kuwa kiwanda kimekuwa kikizalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa ujenzi wa nyumba.
Amesema kuwa kiwanda hicho kimeweka mikakati ya kutoa ajira kwa watanzania zaidi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa bora kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akielezea manufaa ya kiwanda hicho, Marandu amesema kuwa ni pamoja na kununua malighafi kutoka katika mikoa ya Lindi, Morogoro, Pwani, na Dodoma kwa asilimia 96 huku asilimia 4 ya malighafi ikitokea China.
Amesema kuwa manufaa mengine ni pamoja na kutoa ajira kwa watanzania wengi huku wakiendelea kulipa kodi mbalimbali Serikalini.
Ametaja manufaa mengine kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Mkiu, Kituo cha Huduma cha Mkuranga ambapo wamejenga wodi ya wazazi na ujenzi wa kituo cha polisi Mkuranga.
Naye Meneja Masoko wa kiwanda hicho, Salum Zuberi akielezea mwenendo wa soko la vigae vinavyozalishwa na kiwanda hicho amesema kuwa wamekuwa wakiuza bidhaa nchini Tanzania na katika nchi nyingine jirani za Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.
Naye Mkaguzi wa Madini katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Muhsin Mustapha akielezea namna Serikali inavyokusanya mapato kutokana na uwepo wa kiwanda hicho amesema kuwa wamekuwa wakisimamia kwa karibu kwa kuangalia mwenendo mzima wa malighafi zinazoingizwa katika kiwanda hicho na kuhakikisha kunakuwepo na nyaraka zote zinazohitajika kisheria.
No comments:
Post a Comment