HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 12, 2021

Wafanyabiashara, Wajasiriamali na Mamlaka za Mitaa wahamasishwa kushiriki Maonesho ya SabaSaba


Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo.

 

Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Wafanyabiashara, Wajasiriamali pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa wamehamasishwa kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya SabaSaba yanayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Kitila Mkumbo wakati akitoa taatifa ya kuanza Maandalizi ya Maonesho hayo.

Amesema kuwa Maonesho ya SabaSaba yana lengo la kutoa fursa za kibiashara na uwekezaji na kwamba ushiriki wao utawaongezea wigo wa kujitangaza na kupata masoko ya bidhaa zao.

'' Tumewaita hapa kuwatangazia maandalizi ya Maonesho tunawahimiza washiriki kuchangamkia fursa hii ya kibiashara na uwekezaji,'' amesema Dkt. Mkumbo.

Amebainisha kuwa washiriki watapata fursa ya kubadilishana katika uzalishaji wa bidhaa huku na kutangaza fursa za uwekezaji.

Ameongeza kuwa Maonesho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Maendeleo Endelevu.

Amefafanua kuwa mwaka huu nchi tano zimethibitisha kushiriki ikiwemo Kenya, China na Pakistani na kusisitiza Makampuni 54 ya nje na 2803 ya ndani yatashiriki.

Pia amesema katika Maonesho kutatengwa mitaa ikiwemo Mtaa wa Kilimo ukionesha bidhaa za kilimo, Mtaa Madini utaonesha bidhaa za madini pamoja na Mtaa wa Wajasiriamali na Viwanda Vidogovidogo ambao utasimamiwa na Shirika LA Viwanda Vidogovidogo(SIDO).

Waziri Mkumbo amesema kutafanyika mikutano ya mitandao yenye lengo kutangaza bidhaa na fursa za uwekezaji na kwamba usajili kwa washiriki kupitia tovuti ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Edwin Rutageruka amesema Maonesho yatakuwa na mabanda ya walemavu hivyo amevisisitiza vyama vyao vichangamkie fursa ya kutangaza bidhaa zao kwani wataunganishwa na mitandao wafanye biashara.

Amesema tahadhari ya Ugonjwa wa Covid-19 zitaendelea kuchukuliwa na kwamba viingilio havitabadilika wakubwa watalipa Sh 3,000, watoto Sh 1,000 huku siku ya Maonesho wakubwa watatoa Sh 4,000.

Aidha, amesema ada za mabanda hazijabadilika ambapo kiwango cha chini kwa Wajasiriamali watatoa Sh 200,000 huku washiriki kutoka nje ya nchi watatozwa Dola 1600.


No comments:

Post a Comment

Pages