HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 30, 2021

WAITARA ATAKA TATHMINI MV MBEYA II

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akishuka katika chelezo kilichopo bandari ya Kiwira, mara baada ya kukagua chelezo hicho wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

 

 

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara, amezitaka taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Wakala wa Meli (TASAC), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kufanya tathmini ya kina kabla ya kuanza matengenezo ya meli ya MV Mbeya II.

 

Ametoa kauli hiyo wilayani Kyela baada ya kukagua miundombinu katika bandari za Kiwira na Itungi na kubaini ucheleweshaji wa matengenezo ya Meli hiyo iliyosimama kutoa huduma katika Ziwa Nyasa mapema mwezi Aprili kutokana na hitilafu za kifundi.

 

“Meli hii imesimama zaidi ya wiki tatu sasa na ninajua meli hii bado iko kwenye muda wa uangalizi hivyo ninawaagiza TPA, TASAC, DMI na Kampuni ya Songoro kukaa na kuwasilisha ripoti haraka iwezekaavyo ili matengenezo yaanze” ameagiza Naibu Waziri Waitara.

 

Naibu Waziri Waitara amesema fedha za Serikali zilizowekezwa kwenye ujenzi wa meli zilirahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wananchi wanaozunguka Ziwa Nyasa kwa nchi za jirani na kuitaka TPA kurejesha huduma mapema iwezekanavyo.

 

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Waitara imeitaka Kampuni ya Songoro Marine kufanya tathmini ya Chelezo ambayo imekuwa bandarini Kiwira kwa zaidi ya mwaka bila kufanyiwa matengenezo  ili kujiridhisha na ufanisi wake kabla ya kupandisha meli zinazohitaji matengenezo.

 

Akiwasilisha taarifa yake kwa Naibu Waziri Waitara Kaimu Meneja wa Bandari katika Ziwa Nyasa Abdallah Mohammed amesema  kuwa tangu kuanza kutumika kwa meli ya MV. MBEYA II kumekuwa na changamoto mbalimbali za kiufundi ambazo Mamlaka imekuwa ikielekeza Kampuni ya Songoro kuzirekebisha.

 

“Mamlaka ya Bandari ilileta wataalamu kukagua Meli hii na walibaini kuwepo kwa hitilafu kwenye baadhi ya mifumo na imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara”. Amesema Mohamed.

 

Meli ya MV Mbeya II ni moja ya meli tatu ambazo zimejengwa na TPA kwa fedha za ndani lengo likiwa ni kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo Ziwa Nyasa, meli nyingine ni pamoja na MV. RUVUMA na MV. NJOMBE.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


No comments:

Post a Comment

Pages