HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 21, 2021

ACT Wazalendo yalitaka Bunge kupitia upya sheria ya tozo za majengo na miamala ya simu


 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chama cha ACT Wazalendo kimelitaka Bunge kurejea upya uamuzi wake wa kupitisha sheria ya utozaji kodi ya majengo kupitia mita za umeme za luku pamoja na ongezeko la tozo za miamala ya simu.

Kimesema tozo hizo ni sawa na ukatili kwakuwa zinakwenda kunyonya mwananchi kwa kumfanya aishi kwa unyonge mkubwa.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 21,2021, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema uamuzi wa Serikali kutoza kodi za majengo kupitia mita za luku  pamoja na tozo kwenye miamala ya simu ni kuwaumiza wananchi masikini.

Amesema si vema serikali kuwatwisha mzigo mkubwa wananchi kutekeleza miradi yake mikubwa ambayo tangu awali haikuridhiwa na wananchi.

Ado amesema Chama cha ACT Wazalendo kilitoa msimamo wa kupingana na hatua ya Serikali, kupitia Bajeti ya Mwaka 2021/2022 kukusanya kodi ya majengo kupitia luku za umeme.

"Tuliweka bayana kuwa hatua hii ya Serikali inakusudia kuwapora fedha mamilioni ya Watanzania  ambao hawahusiani hata kidogo na kodi ya majengo kwa sababu hawamiliki.

 "Tulidhani kuwa kwa hoja hii, Serikali ingetafakari upya kodi hii hasa kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka bayana kwenye hotuba zake za awali kuwa hapendi kodi za dhulma. Kodi ya majengo kwa kutumia luku ni wizi wa mchana kweupe wa dola kwa wananchi wake." Amesema Ado.

Aidha Katibu Mkuu huyo wa ACT Wazalendo amesema baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa taarifa kwa umma juzi Agosti 19 2021 kuhusu kuanza kwa kodi ya majengo kwa kupitia mfumo wa luku, jana tarehe 20 Agosti 2021, chama  kilichukua hatua kwa kumuandikia barua ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutaka ufafanuzi wa namna TRA itakavyohakikisha kuwa wapangaji hawaguswi na kodi hii kwa vile hawamiliki majengo."

"Pia, Serikali ilipaswa kwanza kabla ya kuanza kukusanya fedha ifanye utambuzi wa luku zinazopaswa kukatwa kodi hiyo ili kuepusha kukata watu kodi kimakosa. Tabia hii ya Serikali kukimbilia kukusanya fedha bila kuweka mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi usio na dhuluma haipaswi.

Aidha ACT Wazalendo imetoa mapendekezo kwa serikali isitishe mara moja zoezi la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa kutumia mita za luku hadi hapo TRA itakapofanya utambuzi wa mita zinazostahili kukatwa.

Mbali na hilo, chama hicho kimeishauri Serikali ijibidiishe kutafuta vyanzo mbadala vya kodi badala ya kumtwisha mzigo mzito mwananchi wa kawaida.

"Mathalani, ACT Wazalendo, kupitia ukurasa wa 47 na 48 wa Ilani yetu, tumeainisha vyanzo mbadala vya kukusanya kodi kuiwezesha Serikali kukusanya mapato bila kuumiza wananchi.

"Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lifanye mapitio (review) ya kodi ya majengo kupitia luku na tozo ya  miamala ya simu ili kuwaondolea mzigo mzito wa kodi wananchi masikini.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

Pages