Baadhi ya washiriki wa CRDB Marathon wakiwa katika mbio za utambuzi wa njia zilizofanyika mwishoni mwa wiki.
Na Upendo Kombe, Dar es Salaam
Maandalizi ya mbio za CRDB Marathon 2021 yamezidi kupamba moto ambapo waandaaji wa mbio hizo wamezitambulisha rasmi njia zitakazotumika kwa washiriki.
Akizungumza wakati wa kutambulisha njia hizo Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kiondo, amesema "leo tupo katika maeneo ya Masaki Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya kuelekea siku ya kusambaza tabasamu ambayo ni siku ya CRDB Bank Marathon zitakazofanyika Agosti 15, 2021, kilichokuwa kinafanyika ni kuweza kuwakusanya wakimbiaji ili waweza kuzifahamu njia zitakazotumika kwa ajili ya mbizo hizo.
"Mwaka huu tupo kimataifa zaidi kwa hiyo tulienda kuwaonyesha mwaka jana tulivyoanza tulikuwa wangali wadogo tumeweza kuwaita wataalamu kutoka nje ya nchi ambao walikuja kurise njia zetu kwa hivyo tukaona ni vizuri kuwakusanya wakimbiaji watakaoshiriki ili waweze kuzifahamu njia ili siku zitakapofanyika mbio zenyewe waweze kujua wapi zitapita". alisema Kiondo.
Ameongeza kuwa usajili wa mbio hizo ulikuwa ufungwe rasmi Julai 30, lakini kutokana na maombi mengi waliyopokea kutoka ndani na nje ya nchi wamelazimika kuongeza siku za kujisajili hadi Agosti 10 ili waweze kupata fursa ya kuungana na Benki ya CRDB pamoja na washirika mbalimbali katika kuhakikisha kwamba wanakwenda kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia maeneo ya kijamii.
Mbio hizo zimelenga kukusanya milioni 500 ambazo zitakwenda kusaidia maeneo matatu ikiwemo Watoto wanaopata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kujenga kituo cha kisasa cha mawasiliano katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambacho kitawasaidia wagonjwa kuweka miadi ya kuonana na madaktari wakiwa hukohuko mikoani kitu ambacho kitawasaidia kuokoa muda na gharama bila ya kufika Dar es Salaam pamoja na kushiriki zoezi la upandaji miti takribani milioni moja nchi nzima.
Mbio za mwaka jana ziliweza kukusanya shilingi milioni 200 ambazo zilisaidia watoto 100 kupata matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Mbio za mwaka huu zitawashirikisha washiriki kutoka mataifa ya Kenya, Zimbabwe, Rwanda, Afrika Kusini na Lebanon, ni wakati sasa ambapo CRDB Bank Marathon inauleta ulimwengu pamoja na kusambaza tabasamu kwa jamii yetu.
Naye mkimbiaji maarufu jijini Dar es Salaam Jovin Vitalis aliyeshiriki katika utambulisho wa njia hizo alisema alikimbia kilomita 21 "faida za mbio hizi ni kuimarisha afya lakini
pia ni msaada mkubwa katika jamii huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa Marathon hizo yenye mchango mkubwa
katika sekta ya afya nchini."Alisema Vitalis.
CRDB Bank Marathon imethibitishwa kufikia viwango vya Kimataifa na Chama cha Mbio za Kimataifa (AIMS) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Riadha (World Athletics).
No comments:
Post a Comment