Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amewataka wakaazi wa Micheweni na Wazanzibari kwa ujumla kudumisha umoja na mshikamano katika jamii zao.
Othman ameyasema hayo akiwa katika ziara maalum katika kijiji cha Micheweni yenye lengo la kusalimiana na kutambuana na majirani zake ambao wanaishi katika kijiji hicho.
Akiwa ameambatana na mke wake, Bi. Zainab Kombo Shaib, na mwenyeji wao Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mohammed Mussa Seif, walitembelea maeneo kadhaa ikiwemo sokoni, majumbani na kwenda kujitambulisha rasmi kwa Sheha wa Shehia ya Majenzi, Ndugu Faki Kombo Hamad.
Aidha Othman amewasisitiza wananchi hao kuweka pembeni itikadi za vyama vyao vya kisiasa na badala yake kuungana kwa pamoja katika kuleta maendeleo.
"Mimi ni kiongozi wenu na nina jukumu la kuwatumikia nyote bila kuangalia itikadi zenu. Nanyi nawasihi sana kulidumisha hilo kwa maslahi mapana ya kijiji chetu na kizazi kinachotuangalia", alisema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais.
Naye Sheha wa Shehia ya Majenzi, Ndugu Faki, amemshukuru Makamu wa Kwanza kwa ziara hiyo na kumueleza kwamba ameonesha mfano bora wa kuigwa wa kuthamini raia wake.
No comments:
Post a Comment