Watendaji wa
Benki ya NMB, wakiwa katika picha wa pamoja na wanafunzi wa skuli ya
Msingi Binguni baada ya benki hiyo kukabidhi msaada wa vifaa vya
kuezekea
skuli hiyo huko Binguni.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi (katikati) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja - Hadidi Rashid Hadidi, msaada wa vitanda vya hospitali vilivyotolewa na benki hiyo kwa baadhi ya hospitali za Mkoa Kusini Unguja huko Binguni.
Na Mwandishi Wetu
Katika kuhakikisha shamra shamra za Siku ya Kizimkazi visiwani Zanzibar zinafana, Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa vya hospitali na shule vyenye thamani ya Shilingi Milioni 54 ili kuwapa tabasamu wakazi wa Kizimkazi katika kipindi hiki.
NMB imetoa jumla ya vitanda 42 ambapo kati ya hivyo vipo vya kujifungulia, vya kufanyia uchunguzi na vya kulalia wagonjwa wodini; vilivyoenda katika Vituo vya Afya saba ikiwemo Bumbwini, Walezo Jeshini, Kizimbani, Chuini, Mwera, Chwaka na Unguja Ukuu pamoja na mabati yaliopelekwa kukamilisha ujenzi wa madarasa ya shule za Kizimkazi, Makunduchi na Binguni zilizopo mkoa wa Kusini na Shule za Mbuzini na Mtoni Kigomeni za Mjini Magharibi.
Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara za Kati wa NMB, Filbert Mponzi alisema kuwa NMB imekuwa ikitenga sehemu ya faida na kuirudisha kwa jamii huku akibainisha kuwa mbali na misaada hiyo NMB wamekua wakitoa elimu ya kutunza fedha kwa wanafunzi wa shule mbali mbali, ambayo inawafahamisha namna ya kutumia na kutunza fedha kwa maisha ya baadae.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, ameipongeza Benki ya NMB kwa misaada mbalimbali wanayoendelea kutoa kwa jamii ya wananchi wa Zanzibar na kuwaomba kutochoka kutoa misaada visiwani Zanzibar.
Aidha, Benki ya NMB imekuwa mdhamini mkuu wa kikao kazi cha mwaka cha Jeshi la Polisi kilichofanyika katika bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbey jijini Dar es Salaam ambapo kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. George Simbachawene, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro na Wakuu wengine wa Majeshi mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment