Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara akifungua rasmi kongamano la tatu la ustahimilivu wa miundombinu leo jijini Dar es Salaam.
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara amesema miundombinu ya barabara, umeme, mawasiliano, maji na reli nchini itadumu kwa muda mrefu ikiwa wajenzi wa miundombinu hiyo watashirikiana wakati wa ujenzi wake.
Akifungua Kongamano la tatu la Ustahimilivu wa miundombinu jijini Dar es Salaam, Mhe. Waitara amesema ujenzi wa miundombinu shirikishi ndio suluhisho la miundombinu bora wakati wote.
“Hakikisheni wajenzi wa barabara, reli, umeme, miradi ya maji na mawasiliano mnawasiliana tangu hatua ya mipango ili miundombinu ya aina moja isiharibu miundombinu ya aina nyingine na kuisababishia Serikali gharama zinazojirudia,” amesema Mhe. Waitara.
Amesisitiza kuwa taasisi zinazojenga miundombinu zikishirikiana katika hatua zote zinaweza kujenga miradi yao kwa pamoja na kwa gharama nafuu zaidi na hivyo kuondoa usumbufu na uharibifu wa miundombinu.
“Nawapongeza kwa kuandaa kongamano hili la wadau wa miundombinu natarajia mtatoka na suluhisho la kudumu katika ujenzi wa miundombinu na kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kujenga na kuikarabati mara kwa mara,” amesisitiza Naibu Waziri Waitara.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini, Dk. Bonifasi Nobeji amesema ushirikishwaji wa wajenzi wa miundombinu unachangia ufanisi katika mnyororo wa thamani katika huduma za uchukuzi na ugavi na hivyo kuisaidia sekta ya bandari kufanya kazi kwa tija.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya B & F Global, Bw. Bruno Kinyaga amesema
kongamano hilo la siku tatu linalowaweka pamoja wadau wa miundombinu linalengo
la kupitia changamoto zilizopo sasa na kutafuta suluhu ya sasa na siku zijazo
katika sekta ya miundombinu.
No comments:
Post a Comment