HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 13, 2021

Steve Nyerere awaasa wananchi kupuuza upotoshaji Chanjo ya Covid-19, awahamasisha kujitokeza kupatiwa chanjo

 Msanii wa Maigizo Nchini Steve Nyerere, akizungumza na waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka.
 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Msanii wa Maigizo Nchini Steve Nyerere amewaomba wananchi kuachana na habari za upotoshaji zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuhusu Chanjo ya Virusi vya Corona (COVID-19) badala yake wajitokeze kwa wingi  kushiriki mchakato wa kupatiwa chanjo hiyo. 

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari  kuhusu upotoshaji unaofanyika kwenye mitandao hiyo ambapo amesema kumekuwepo na habari zinazohamasisha watu kukataa chanjo hiyo inayotolewa kwa hiari na si lazima.

Amebainisha kuwa katika mitandao hiyo kuna upotoshaji unaowataka wananchi kukataa kuchanjwa chanjo ya Johnson Johnson na kwamba ni vyema waache vitendo kwani ni hiari ya mtu. 

"Sisi tumechanjwa ila kuna watu wanawashwa washwa watakunwa  waache kutumia mitandao ya kijamii kupotosha na kuleta taharuki," amesema Nyerere.

Msanii huyo amewahamasisha vijana nchi nzima kujitokeza wapatiwe chanjo hiyo wajikinge na wimbi la tatu la ugonjwa  wa Covid-19 ambao umeripotiwa kusababisha vifo vingi duniani.  

Ameongeza kuwa Samia Suluhu Hassan  amekuwa mfano mzuri katika kutekelezamchakato wa kupatiwa hivyo ni vyema wananchi wakamuunga mkono kujihadhari na ugonjwa huo. 

Kwa upande wake Abdallah Mkumbila 'Muhogo Mchungu' amesema kuna vitendo vya upotoshaji vinavyofanyika mitandaoni kuhusu ugonjwa wa corona hivyo ni vyema wapotoshaji wakatambua ugonjwa huo upo na kuchukua tahadhari.

Naye  Mkurugenzi wa Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka amesema wasanii ni vioo vya jamii hivyo yuko tayari  na Wasanii wenzake kuzunguka nchi nzima kutoa elimu ya umuhimu na faida ya kuchanjwa japokuwa inatolewa kwa hiari.


No comments:

Post a Comment

Pages