HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 14, 2021

WAKANDARASI WANAWAKE WATAKIWA KUJITUMA

 

Meneja wa Bodi ya Wakandarasi (CRB), kanda ya Mwanza Mkadiriaji Majenzi, Godfrey Kazi akimkabidhi cheti cha uhitimu wa mafunzo ya teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi wa barabara mhitimu Prisila Kapinga kutoka mkoa wa Geita.

Picha ya pamoja ya Wakandarasi wanawake kutoka Mkoa wa Simiyu mara baada ya kuhitimu mafunzo ya ukandarasi kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi wa barabara yalioandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Jijini Mwanza.

 

 Na Mwandishi Wetu

Meneja wa Bodi ya usajili wa Wakandarasi (CRB), Kanda ya Mwanza Mkadiriaji Majenzi Godfrey Kazi amesema Serikali itazielekeza taasisi nunuzi zote kutenga kazi kwa makundi maalum wakiwepo wanawake ili kuwezesha usawa katika miradi ya ujenzi wa barabara nchini.

Akifunga mafunzo ya wiki mbili ya wakandarasi wanawake wanaotumia teknolojia stahiki ya nguvukazi katika ujenzi wa barabara jijini Mwanza Meneja huyo amesisitiza umuhimu wa wakandarasi wanawake kufanyakazi kwa bidii na nidhamu ili wapewe miradi mingi na hivyo kukuza katika fani ya ukandarasi.

“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), imedhamiria kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa barabara ili kufuata sera zilizopo na kuwakomboa kiuchumi”, amesema mkadiriaji majenzi Kazi.

Amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaendelea kuhamasisha wanawake kushiriki katika kazi za ujenzi wa barabara ili kuongeza tija kwa wanawake wenyewe na kuondoa dhana kuwa kazi hizo ni kwaajili ya wanaume pekee.

Kwa upande wao washiriki waliohitimu mafunzo hayo wameiomba Serikali kuendelea kuwapa fursa zaidi katika kazi za barabara ili kuwajengea uwezo na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi binafsi na wa taifa.

Zaidi ya wanawake 80, kutoka katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Mara na Kagera wameshiriki katika mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha wanawake wakandarasi kushiriki katika ujenzi wa barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi.

No comments:

Post a Comment

Pages