Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, akitia saini kanuni za uendelezaji wa nishati mbadala.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro akikata utepe ili kuzindua kanuni za uendelezaji wa nishati mbadala. Wengine ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki kulia Dk.Ezekiel Mwakalukwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Do Santos Silayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas
Ndumbaro akizungumza na wananchi baada ya kutia saini kanuni za
uendelezaji wa nishati mbadala.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii Dk. Damas Ndumbaro amewataka Watanzania
kujipanga kutumia nishati ya mkaa mbadala ili kuendelea kuilinda misitu
isiharibiwe.
Wito huo
ameutoa wakati akizindua mkakati wa utekelezaji wa sera ya misitu ya
(1998) na utiaji saini wa kanuni za uendelezaji wa nishati ya mkaa
mbadala uliofanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea Mkoani
Ruvuma.
Dk.Damas Ndumbaro
ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani humo amesema kuwa
Watanzania hasa waishio mijini wakitumia mkaa mbadala basi misitu
itaendelea kuwa salama na kuvifanya viumbe vinavyoishi kwenye misitu
hiyo viendelee kuongezeka kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
Waziri
huyo amesema kuwa hadi sasa hapa nchini wafanyabiashara 19 wameanzisha
viwanda vya kuchakatia nishati ya mkaa mbadala hivyo kupitia kanuni
zilizosainiwa zitawasaidia kupata uwezo wa masoko ndani na nje ya nchi
hivyo kuifanya ajira iweze kuongezeka.
Kwa
upande wake Kamishina wa Uhifadhi wa Wakala wa Huruma za Misitu (TFS),
Profesa Dos Santos Silayo amesema kuwa mkaa mbadala unapatikana kwa
masalia ya miti na mabaki ya mimea mbalimbali ikiwemo mazao yanayolimwa
na Wananchi.
Profesa
Silayo amesema kuwa licha ya kulinda misitu lakini bado hata mwananchi
ambaye ni mkulima bado atanufaika na mabaki ya mimea ya mazao yake kwa
kuwa anaweza akayauza na kisha kumuingizia kipato cha fedha.
Mkurugenzi
wa Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.Ezekiel
Mwakalukwa amesema kuwa mkaa ni zao moja wapo linalotokana na mazao ya
misitu hivyo utumiaji wa mkaa mbadala utawasaidia pia wananchi kutambua
faida za matumizi ya mkaa huo.
Utiaji
saini huo ambao umeenda sambamba na maadhimisho ya Majimaji selebuka
,umehudhuliwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali pamoja na
baadhi ya wakazi wa mjini Songea ambao wengi wao wamedai wamenufaika na
mpango huo wa matumizi ya nishati ya mkaa mbadala.
No comments:
Post a Comment