HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 14, 2021

Balozi Finland afurahishwa na TAMWA-ZNZ

 


Naibu Balozi wa Finland Nchini Tanzania Sari Ussi Rauva(katikati) akisisitiza jambo wakati alipokua akizungumza na Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt, Mzuri Issa (kulia) na Asna Mshana ambaye ni mratibu wa miradi kutoka ubalozi wa Finland nchini Tanzania.


Naibu Balozi wa Finland Nchini Tanzania Sari Ussi Rauva akizungumza mara baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya utekelezaji mradi katika ofisi za TAMWA-ZNZ Tunguu Wilaya ya kati Unguja.


Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.


Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wakifuatilia uwasilishwaji wa ripoti hio.

 

Na Talib Ussi Zanzibar

Naibu Balozi wa Finland Nchini Tanzania Sari Ussi Rauva ameleza kufarijika kwake matumizi ya rasilimali walizozipatia TAMWA-ZNZ katika kuongeza kasi dhidi ya mapambano ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto visiwani Zanzibar.

 

Aliyasema hayo katika ukumbi wa TAMWA-ZNZ Tunguu Wilaya ya kati Unguja mara baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya utekelezaji wa mradi wa kupambana na matendo ya dhalilishaji visiwani hapa.

 

Alisema wao kama ofisi ya ubalozi wa Finland Nchini Tanzania  wanajivunia kufanya kazi na TAMWA katika kipindi chote cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huo kwani umeonesha mabadiliko makubwa kwenye jamii.

 

Alisema kupitia ripoti hio  ni faraja kubwa kuona watu wanazungumza mafanikio ya utekelezaji mradi huo ikiwemo watoto wao kutoa ushahidi na hatimae waliohusika kutiwa hatiani.

 

Awali akikaribisha ugeni huo Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt Mzuri Issa alisema kabla ya kutekezwa kwa mradi huo wa kuwajengea uwezo wazee na wahanga wa matukio ya udhalilishaji ilikua ngumu sana baadhi yao kufika mahakamani na kutoa ushahidi.


Alisema kupitia mradi huo wahanga wa udhailishaji walijengewa uwezo na hatimae kutoa ushahidi mbele ya Mahakama bila ya kuwa na chembe ya hofu,na kupelekea watendaji wengi wamatukio hayo kuhukumiwa.

 

Kwa upande wake Afisa utafiti na tathmini TAMWA-ZNZ Mohamed Khatib alisema mradi huo wa miaka mitatu kutoka mwaka 2019-2021 ulikusanya makundi mbali mbali yakiwemo ya wazazi wa wahanga,watoto wao pamoja na baadhi ya waandishi wa habari huku lengo likikuwa ni kuwajengea uwezo kuhusu pambano dhidi ya matendo ya udhalilishaji.

 

Alisema awali mradi huo ulilenga kuwafikia wanufaika wapatao 12,000 lakini walivuuka lengo hilo na kuwafikia watu wapatao 15,000 katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

 

Alisema jitihada kubwa zilifanyika za kuwajengea wanufaika wa mradi huo uwezo wa kusimama na kutoa ushahidi unaotakiwa sambamba na kufuatilia kesi zao huku kwa upande wa waandishi wa habari kutambua njia bora za kuripoti na kufanya mwendelezo wa habari wanazozitoa.

 

Akiendelea kufafanua zaidi Afisa huyo alisema katika kipindi chote cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi huo kesi zipatazo 1377 ziliriripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi na kuzifuatilia na  idadi kubwa ya kesi hizo zilikua ni za kubaka ambazo ni 403 na kwa upande wa kesi  zilizopatiwa hukumu zilikua ni kesi 163 na kesi ambazo zipo vituo vya polisi ni 581,mahakamani  198 na kesi zilizofutwa kwa sababu mbali mbali ni 92.

 

Wakitoa ushuhuda baadhi ya wazazi ambao watoto wao walikutwa na kadhia hio ya udhalilishaji mmoja miongoni mwa mzazi alisema bila ya kupewa elimu na TAMWA kupitia mradi huo asingeweza kufuatilia kesi yake.

 

Alisema kupitia elimu hio ilimjenga ujasiri yeye na mtoto wake ambae awali alikua akishindwa kutoa udhahidi lakini mara baada ya elimu hio alikua jasiri na kusimama mahakamani mwenyewe bila ya woga .

 

Alisema kupitia ujasiri huo mtoto wake alitoa ushahidi  licha ya uwepo wa vitishho na hatimae aliemtendea unyama huo mtoto wake alitiwa hatiani na mahakama na  kufungwa miaka 30 chuo cha mafunzo.

 

Sambamba na hayo akitaja miongoni mwa faida nyengine alisema mtoto wake huyo kutokua na wasiwasi na sasa anaedelea na masomo yake kama kawaida na kwa bahati nzuri mwaka huu ametokea wakwanza darasani kwao.

No comments:

Post a Comment

Pages