Na Lydia Lugakila, Bukoba
Kufuatia agizo lililotolewa na mbunge wa Bukoba na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato alilolitoa julai 30 mwaka huu la kulitaka shirika la umeme TANESCO Mkoani Kagera kuhakikisha linafikisha huduma ya umeme katika eneo la Kazinga lililopo kata Bakoba mtaa Kafuti manispaa ya Bukoba kabla ya Novemba mwaka huu tayari limefanikiwa na taratibu za kuunganishiwa umeme limeanza.
Akizungumzia hatua hiyo Afisa uhusiano na huduma kwa wateja kutoka shirika hilo Samweli Mandale amesema kupitia kampeni maalum ya kusogeza huduma ya umeme karibu na wananchi ijulikanayo Kama "OBUMEME TWABULETA imelenga kuwasogezea wateja huduma katika baadhi ya maeneo yote ya ukanda wa kijani Bukoba, ambapo tayari eneo la Kazinga utekelezaji na taratibu za kuunganishiwa umeme limeanza na kuwataka wananchi kupokea mradi huo na kuchangamkia fursa zitokanazo na nishati ya umeme.
"Sisi TANESCO tunasema tayari huduma imefika na taratibu za kuunganishiwa umeme ni nyepesi sana hivyo Kufuatia maelekezo ya Mbunge Byabato juu ya kuwafuata wateja walipo tumelitimiza nashukuru mbunge kwa kuwajali wananchi pia niwaombe mkachangamkie fursa hiyo kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo, anzisheni viwanda vya kukoboa nafaka, tumieni nishati hii kuwaletea maendeleo alisema Mandale".
Mandale amesema shirika hilo limejidhatiti kutoa elimu juu ya miradi ya umeme na kuwa hadi sasa tayari wamefanikiwa kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo ikiwemo Kagondo Kaluguru, Buhembe, Mafumbo Rwome na Sasa Kazinga na kuwa maeneo mengine mafundi wanaendelea na kazi ambapo ameongeza kuwa kabla ya Novemba mwaka huu umeme utafika maeneo yote manispaa ya Bukoba, huku akisisitiza gharama ya umeme kuwa ni shilingi elfu 27 tu.
Kwa upande wake Mhandisi Pasaka Bakari ambaye ni katibu wa mbunge wa Jimbo la Bukoba kwa niaba ya mbunge amewataka wananchi hao kumuamini mbunge wao kwani moja ya ahadi yake imetimizwa huku akiwataka kuitunza na kuilinda miundombinu na kushirikiana kupokea miradi ya umeme ili iweze kuwaletea manufaa.
Naye diwani wa kata ya Bakoba Shaban Rashid amewaomba wananchi kutoa ushirikiano inapokuja miradi ya maendeleo katika maeneo yao, huku akiwataka wananchi waliowekeza vichaka na misitu kuondoa vichaka hivyo kabla ya sheria ndogo ndogo za halmashauri ya manispaa ya Bukoba ya mwaka 2018 zinazozuia uwepo wa vichaka na misitu mikubwa kuanza kutumika.
Aidha kwa upande wao baadhi ya wananchi wa maeneo hayo akiwemo Samweli Wambura na Bi Jesca wameishukuru serikali kwa huduma hiyo na kueleza kuwa tangu wamehamia eneo hilo miaka 3 imepita wakiwa hawaamini Kama huduma hiyo ingewafikia.
No comments:
Post a Comment