Na Irene Mark
SIKU 78 baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri uhaba wa mvua za msimu wa vuli, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), linakabiliwa na upungufu kwenye uzalishaji kwa asilimia 21.
TMA ilitabiri kuwepo kwa mvua za chini ya wastani hadi wastani kwa maeneo mengi ya nchi hivyo kuashiria uhaba wa mvua utakaosababisha ukame hapa nchini na kwamba hali hiyo itapungua baada ya Machi, 2022.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Novemba 18,2021 na Ofisi ya Uhusiano ya Tanesco Makao Makuu, imeeleza kwamba kuna upungufu wa maji kwenye mabwawa na mito inayozalisha umeme hapa nchini.
“Hali ya kiwango cha maji kwenye mabwawa na mito kimepungua kwa kiwango kikubwa na kuathiri uzalishaji wa umeme kwenye vituo vyetu vya Kihansi, Kidatu na Pangani.
“...Jumla ya upungufu wa uzalishaji ni takribani 345MW sawa na asilimia 21 ya uzalishaji wetu wote,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco inachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asili na kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo.
“Mitambo inayotengenezwa ni Ubungo 1 (25MW), upanuzi wa Kinyerezi I (185MW) na Ubungo III (112) na kuwasha kituo cha Nyakato (36MW). Hii itaongeza jumla ya 358MW,” inaeleza taarifa hiyo kwa umma.
Hata hivyo imebainishwa kwamba taarifa za upungufu wa umeme kwenye baadhi ya mikoa zitatolewa zitatolewa kwa wakati ili wananchi wajipange kukabiliana na upungufu huo.
No comments:
Post a Comment