HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 30, 2021

ROSE MANUMBA TRUST YAWAPA NEEMA VIJANA 11 KUTOKA VETA


*Wahimizwa kutumia fursa ya mkopo inayotolewa katika Halmashauri nchini

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Rose Manumba Trust kwa kushirikiana na Give A Future Foundation kupitia program ya 'Jiajiri' wamekabidhi vifaa vya ufundi kwa wanafunzi kumi na moja waliopata mafunzo kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafuzo ya Ufundi stadi VETA Chang'mbe, Donbosco na St. Gasper ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi, kujiajiri pamoja na kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto ya ajira nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa vijana hao wanaosomea fani za ufundi cherehani, ufundi umeme, mapishi na urembo Katibu tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala Charangwa Seleman amesema Serikali inatambua juhudi za wadau katika kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya ajira hasa kwa kundi la vijana.

''Mkatumie vifaa hivi vya msingi kwa kufanya kazi na kutengeneza ajira, epukeni makundi Serikali na wadau kama Rose Manumba Trust tupo pamoja katika kuhakikisha tunapambana kutatua changamoto ya ajira...Pia mtumie mafunzo ya ujasiriamali mliyopewa kwa ufanisi ili kuwapa moyo wadau hawa na ninaamini mtawainua vijana wengi zaidi kupitia fursa hii mliyoipata.'' Amesema.

Aidha amewataka vijana hao kutumia fursa za mkopo zinazotolewa katika Halmashauri zote nchini kwa makundi ya wanawake ambao hupata asilimia nne, wanaume asilimia nne na wenye ulemavu asilimia mbili.

''Vijana tumieni fursa hii mmepata vifaa msibweteke, pia kuna fursa za mkopo unaotolewa bila riba katika Halmashauri, kwa vifaa mlivyopata mnaweza kuwa na kikundi mkaandika mpango mkakati wa biashara na kuuwasilisha katika Halmashauri zenu,,,kwa wale wanaotoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala nitawasaidia, jitihada za Rose Manumba Trust na Give A Future Foundation tuziendeleza kwa kuwapa moyo ili waweze kuwafikia vijana wengi zaidi.'' Amesema.

Pia amewataka wadau na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa kuunga mkono juhudi hizo kwa kusaidia kundi la vijana hasa katika changamoto ya ajira inayowakabili.

Awali Mkurugenzi wa taasisi ya Rose Manumba Trust, Veronica Mwamunyange amesema taasisi hiyo imelenga kusaidia vijana, wanawake na wenye ulemavu katika kujikwamua kiuchumi na katika sekta za elimu na afya kwa wanawake na vijana.

Amesema wamekuwa na miradi mbalimbali ikiwemo Msichana Club maalum kwa vijana wa kike na programu ya 'Jiajiri' ambayo imewalenga vijana wanaosoma VETA kwa kupatiwa vifaa vitakavyowasaidia mara baada ya kuhitimu masomo yao.

''Taasisi hii iliona changamoto kwa vijana wanaosoma Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kukosa vifaa vya kazi pindi wanapomaliza masomo yao, tukaona ni vyema kufanya mchakato wa kuwasaidia vijana hawa kupitia shindano ambalo lilishirikisha vijana 150 wanasoma kozi zenye uhitaji ambao walijaza fomu na vijana 11 pekee waliingia katika kinyang'anyiro na walipewa mafunzo ya ujasriamali na wapo tayari kuanza biashara mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo.''

Veronica amesema, wataangalia maendeleo ya vjana hao mara baada ya kukabidhiiwa vifaa hivyo na kuwataka vijana hao kuendeleza ujuzi waliupata katika kujikwamua kiuchumi na kuwasaidia wengine.

''Muasis ya taasisi hii Rose Manumba alitamani kuwa nanyi hapa leo lakini amebanwa naa majukumu ya kiserikali ila amefurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya vijana hawa, anawatakia kila la heri katika ujenzi wa taifa ambao kasi yake katika kupambana na changamoto ya ajira inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan inadhihirika wazi.'' Amesema.

Vilevile mshauri wa taasisi hiyo Jestina Kimesa amesema changamoto kubwa inayokwamisha programu za aina hiyo ni utekeleezaji wa miradi husika na kuwataka vijana hao kubadilisha dhana hiyo na kuwapa moyo wanaowasaidia kwa kufaanya kazi kwa bidii na kuwasaidia vijana wengine.

Mwakilishi wa wanufaika hao Issa Mohammed anayesomea mapishi VETA Chang'ombe ameishukuru taasisi ya Rose Manumba Trust kwa kuwapa nyenzo muhimu ambazo zitawasaidia katika kujikwamua kiuchumi na baadaye kuweza kuwasaidia vijana wengine.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Seleman (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Ayenda Ezekiel (kushoto) ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafuzo ya Ufundi stadi (VETA) ya Chang'mbe walionufaika na vifaa vya ufundi kupitia mradi Jiajiri wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Rose Manumba Trust kwa kushirikiana na Give A Future Foundation, katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya ufundi kwa wanafunzi kumi na moja waliopata mafunzo kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafuzo ya Ufundi stadi (VETA) ya Chang'mbe, Donbosco na St. Gasper za Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kujiajiri, iliyofanyika jana kwenye Hoteli ya Kebbs, Dar es salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa taasisi ya Rose Manumba Trust, Veronica Mwamunyange (wa pili kulia) pamoja na Mlezi wa taasisi ya Rose Manumba Trust, Jestina Kimbesa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Seleman akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi kumi na moja waliopata vifaa vya ufundi kupitia mradi Jiajiri wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Rose Manumba Trust kwa kushirikiana na Give A Future Foundation, katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya ufundi kwa wanafunzi kumi na moja waliopata mafunzo kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafuzo ya Ufundi stadi (VETA) ya Chang'mbe, Donbosco na St. Gasper za Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages