HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 30, 2021

SERIKALI YAIAGIZA TAKUKURU KUWEKA MASANDUKU YA MAONI KUHUSU VIASHIRIA VYA RUSHWA KATIKA TAASISI ZA UMMA PAMOJA WIZARA

 Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe.Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa nchini[TAKUKURU]kuhakikisha inaweka masanduku ya maoni kuhusu viashiria vya rushwa katika taasisi zote za serikali pamoja na wizara  ili kuweza kupokea maoni ya wananchi juu ya viashiria vya rushwa katika taasisi hizo.


Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma katika mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa TAKUKURU   ambao unatoa fursa kwa viongozi wa TAKUKURU kutathimni utendaji wa kazi wa mwaka mzima  uliopita  kwa mujibu wa sharia ya kuzuia  na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.


Waziri Mchengerwa amesema viongozi walio wengi hawatambui kuwa nchi ni ya wananchi hivyo TAKUKURU ina nguvu kubwa katika kupambana na viongozi wasio waaminifu.


Hivyo,Waziri Mchengerwa ameiagiza TAKUKURU kuandaa masanduku katika taasisi zote ili kubaini  wapokeaji rushwa katika taasisi hizo huku akibainisha kuwa katika mwaka huu ,serikali imetoa kibali cha ajira  mpya 350  kwa TAKUKURU.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini [TAKUKURU]Kamishna wa  polisi , SALUM RASHID HAMDUNI amesema hadi sasa TAKUKURU imeshashinda kesi  za rushwa 345  na kushindwa kesi 156 huku  ikiokoa Tsh.bilioni 29.3 .


Ikumbukwe kuwa ,mwaka 1971 ilitungwa sheria ya kuzuia Rushwa Na.16  ili kukabili tatizo la rushwa nchini ,baada ya miaka mitatu ,Januari 15,1975  serikali ilianzisha kikosi cha  cha kuzuia rushwa  chenye dhamana ya kutekeleza sharia Na.16/1971   na kilikuwa chini ya jeshi la polisi  na mwaka 1991  sheria ya kuzuia Rushwa Na.16/1971  iliboreshwa    ili iendane na wakati  na ikaitwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa [TAKURU] na wengi walizoea kama PCB ,na ilipofika mwaka 2007  ilibadilishwa kuwa  Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)

 

 Hivyo mabadiliko haya yaliendana na ongezeko la Wigo wa kushughulikia makossa ya rushwa  kutoka makosa  4  na kuwa makossa 24  chini ya sharia ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  Na.11  ya mwaka 2007 inayotumika hadi sasa.



No comments:

Post a Comment

Pages