Na Mwandishi Wetu
Shirika
la Posta la nchini Burundi limeweka bayana dhamira yake ya kushirikiana na
Tanzania katika kukuza sekta ya Posta nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi
zaidi katika usimamizi wa masuala ya Posta.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya posta wa Burundi Bi. Lea Ngabire
wakati alipozuru Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
akiambatana na ujumbe wa Maafisa waandamizi wa Posta Burundi katika ziara ya
mafunzo.
“Tumefika
hapa TCRA na kujionea shughuli mbalimbali za mawasiliano na lengo letu ni kuona
namna nchi zetu mbili zinavyoweza kushirikiana katika kukuza na kuendeleza
sekta ya posta” alibainisha Ngabire.
Ujumbe
wa Maafisa hao umejumuisha Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Posta Burundi
Nyayishimiye Olivier na Mkuu wa masuala ya Barua Misirakuba Deo.
Akipokea
ujumbe huo mnamo Jumatano Tarehe 17 Novemba 2021 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari aliwakaribisha na kuwaeleza kuwa TCRA
kama mdhibiti wa sekta ya Mawasiliano nchini Tanzania inatambua umuhimu wa
ushirikiano wa mawasiliano hasa kikanda na imekuwa mshirika muhimu wa
mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Lengo
letu ni kuhakikisha sekta ya mawasiliano nchini Tanzania inasimamiwa kwa
uthabiti na kwa upande wa posta TCRA imekuwa ikishirikiana na taasisi
mbalimbali za kikanda na kimataifa na kama mnavyofahamu pia Makao Makuu ya
Posta Afrika yapo hapa nchini” alibainisha na kuongeza Jabiri.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akizungumza na ujumbe
wa Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Posta Burundi wakiongozwa na Mkurugenzi
Mkuu wa Posta Burundi Bi. Lea Ngabire walipotembelea
Mamlaka hiyo kwa ziara ya mafunzo. Picha
na: TCRA.
Pembezoni
mwa mazungumzo na ujumbe huo pia, Mkurugenzi Mkuu Jabiri aliwaeleza wajumbe hao
kwamba Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano
barani Afrika inaimarika na ndiyo sababu imekuwa ikishirikiana na Shirika la
Posta Afrika (PAPU) kuhakikisha ujenzi wa Ofisi ya PAPU makao makuu ambayo
ujenzi wake unaendelea jijini Arusha unakamilika kwa wakati ambapo matarajio ni
kukamilisha ujenzi wa jingo la kisasa jijini Arusha itakapowadia 2022.
Nae
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA Dkt. Emmanuel Manasseh ambae sekta ya
Posta inasimamiwa na kurugenzi anayoingoza alibainisha kwamba hakuna namna
uchumi wa kisasa utajengwa bila kuhusisha posta kwani sekta hiyo ni muhimu
katika masuala ya usafirishaji na ufikishaji wa taarifa mbalimbali
zinazowezesha kujenga uchumi wa kisasa (Uchumi wa kidijitali).
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Posta Burundi Bi. Lea Ngabire akisaini Kitabu cha Wageni
wakati alipotembelea Makumbusho ya Mawasiliano iliyopo Makao Makuu ya Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Katika ziara hiyo ya mafunzo Ingabire
aliambatana na Maafisa Waandamizi wa Posta Burundi. Picha na: TCRA.
“Tunapoenda
kwenye uchumi wa kidijitali posta ni sekta muhimu sana ambayo hatuwezi kukwepa
kuitumia kwani itatuwezesha kufikia azma ya kujenga uchumi wa kidijitali.”
Alisisitiza Dkt Manasseh.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo ujumbe huo ulibainisha kufurahishwa na maarifa waliyopata baada ya kutembelea TCRA ili kujifunza na kuahidi kwamba watatendea kazi yale waliyojifunza katika kukuza sekta ya Posta nchini Burundi.
No comments:
Post a Comment