Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, amesema atawaombea kazi katika mradi wa bomba la mafuta
mafundi wote wanaosimamia ujenzi wa miradi ya shule na vituo vya afya vinavyogharimiwa na fedha za Uviko-19 na tozo za mihamala ya simu, mkoani hapa.
Amesema ahadi hiyo ataitekeleza kwa mafundi waadilifu wanaosimamia miradi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na kuikabidhi kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza katika Shule ya Sekondari Jaila wilayani Mkinga akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi hiyo, Malima amesema mafundi waliozembea ahadi haiwahusu.
Aidha, akiwa shuleni hapo Malima ametoa siku 10 kwa fundi anayesimamia ujenzi huo awe amepaua majengo mawili ya madarasa ambayo yako katika hatua ya msingi.
"Ikifika tarehe 16, uwe umepaua majengo yote siku hiyo tutakuja kukagua na tutakapokuja matarajio yetu tutakuta umefikia hatua hiyo ili watoto wakija kuanza shule Januari wakute madarasa tayari," amesema.
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilindi (Kilindi Girls), Malima aliahidi kutoa Sh milioni moja kwa ajili ya kuendeleza ujenzi kwa wananchi watakaojitolea na kuunga mkono mradi wa wasichana utakaoanzishwa.
Pamoja mambo mengine, Malima amesema amesikitishwa na Wilaya ya Kilindi kwa ujumla kufanya vibaya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za Uviko 19 na tozo za mihamala ya simu.
Halmashauri hiyo inaongoza kwa kuwa na miradi mingi ya utekelezaji ambapo kwa wilaya Kilindi pekee ni madarasa 199 huku kwa mkoa mzima wa Tanga madarasa 723.
Aidha, kati ya hiyo mradi mmoja ni Kituo cha Afya Mswaki kukichopo Kata ya Msanja, shule shikizi 10 katika Kata za Negero kwenye shule tano, Songe shule moja, Kibirashi shule mbili na shule moja iko Kata ya Jaila.
Hata hivyo kuna miradi ya shule za sekondari katika kata za Jaila ambako kuna shule tatu, Msanja sekondari moja, Kwediboma shule moja, Songe shule moja, wakati kata ya Lwande shule moja, Kimbe shule moja na Negero kuna shule moja, ambapo shule zote zimepatiwa fedha za Uviko 19.
No comments:
Post a Comment