HABARI MSETO (HEADER)


December 07, 2021

KAMPUNI YA NKUSU THEO SUGAR YASAIDIA VIFAA VYA UJENZI SONGEA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Menas Komba akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe sehemu ya msaada huo.

 

NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

KAMPUNI ya Nkusu Theo Sugar imetoa vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa ajili ya kusaidia ukarabati wa vyumba viwili vya  madarasa katika Shule ya Msingi Nakawale iliyopo Kata ya Muhukuru barabarani Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

 

Afisa Fedha na Tawala wa kampuni hiyo Longanus Kagaruki amevitaja vifaa ambavyo wamevitoa kuwa ni saruji mifuko 100,nondo 24 za milimita 16,ndoo za rangi 10  kati ya hizo ndoo sita za rangi ya mafuta na ndoo nne ni za rangi ya maji na waya kwa ajili ya kuweka kwenye madirisha.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe ameishukuru kampuni hiyo kwakusaidia maendeleo ya kujenga mazingira wezeshi ya kutolea huduma bora za elimu ambayo yatasaidia watoto kusoma na kujifunza vizuri.

 

Maghembe  amesema mazingira bora na mazuri ya kusomea na kujifunzia yanasaidia kuleta maendeleo chanya kwa familia na jamii kwasababu ni chachu ya mafanikio.

 

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matimila Menas Komba amewataka viongozi wa Kijiji kutumia vifaa hivyo kama walivyo viomba ili kuwatia moyo wadau wanaosaidia shughuli za maendeleo ndani ya Halmashauri badala ya kuwakatisha tamaa kwa kutumia misaada hiyo kinyume na taratibu.

 

“Naomba Mwenyekiti wa Kijiji umekabidhiwa vifaa ukavitumie  kama inavyotakiwa na wananchi waambiw”amesisitiza Menas Komba.

 

Komba ametoa rai kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wanaotaka kuwekeza  katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kufika katika Halmashauri hiyo kufanya shughuli za uwekezaji kwa sababu maeneo yapo ya kutosha na hali ya hewa inaruhusu inafaa kwa shughuli hizo.

 

Kampuni ya Nkusu Theo Sugar inatarajia kujenga kiwanda cha kuzalisha sukari katika Kijiji cha Nakawale mapema mwakani 2022 endapo taratibu zote zitakamilika ikiwemo la kupatiwa hati miliki ya maeneo waliyoomba kwa ajili ya kazi hio ,kwasasa kampuni hiyo imeshaanza kulima miwa ekali zipatazo 50 kwa ajili ya uzalishaji wa sukari.

No comments:

Post a Comment

Pages