HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

January 14, 2022

Mtaalam wa kodi ajitosa uspika wa Bunge



Na Irene Mark


KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mtaalam wa Kodi, Hamidu Chamani leo Januari 14.2022 amerudisha fomu ya kugombea uspika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano kwenye ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kurudisha fomu hizo, Chamani amesema anaamini anao uwezo wa kuongoza Bunge na kukisaidia chama chake katika kuleta maendeleo ya nchi kupitia Bunge.

Januari 6,2022 Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kujiuzulu kwenye nafasi hiyo baada ya kuwepo kwa taharuki juu ya utata wa kauli zake juu ya mikopo inayochukuliwa na serikali chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kujiuzulu kwa Ndugai kumetoa nafasi kwa CCM kuruhusu wanaotaka kuwania uspika kupitia chama hicho kuchukua na kurudisha fomu kuanzia Januari 10 hadi 15,2022 ambapo mpaka sasa makada 49 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Chamani aliyepata kuwania ubunge wa jimbo la Kyerwa mkoani Kagera mwaka 2020 amesema idadi kubwa ya waliowania nafasi hiyo haimpi tabu kwa kuwa yeye ni bora zaidi yao.

“Nimefanya kazi za kukitangaza chama tangu mwaka 2010 nimehamasisha vijana wengi wa vyuo vikuu kujiunga na CCM wapo wengin niliowapatia kadi kwa mkono wangu.

“Ninajiamini nakijua chama na nitatumika vema kwenye nafasi ya uspika,” anasema Chamani ambaye kwa sasa ni msimamizi wa mashine za kutolea risiti kwa njia ya kielektroniki jijini Dar es Salaam.

Gharama ya fomu moja ni Sh. Milioni moja, hata hivyo idadi ya makada wanaowania nafasi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Miongoni mwa waliochukua fomu ya kuwania uspika ni Katibu mstaafu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Mfutakamba, Naibu Spika wa sasa, Dk. Tulia Akson na Waziri wa zamani wa Utawala Bora na Mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM, Sophia Simba.


No comments:

Post a Comment

Pages