HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

January 18, 2022

Serikali yagawa pikipiki 300 kwa maafisa ugani nchini

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango (wa pili kushoto), akikata utepe kuashiria kutoa pikipiki ka maafisa Ugani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi mikoa yote ya Tanzania Bara, hafla hiyo imefanyika leo jijini Dodoma, wengine kutoka kushoto ni waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Inoicent Bashunga, waziri wa Mifugo na uvuvi Mashimba Ndaki,Mkuu a Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ulega. Picha na Deus Mhagale.

 

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango  (kushoto), akiwasha pikipiki kabla ya kuzigawa jana kwa maafisa ugani wa wizara ya Mifugo na Uvuvi.

 

 

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, akimkabidhi ufunguo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka.

 

 

Waziri Mashimba Ndaki na Naibu wa wizara hiyo Abdallah Ulega, wakibadilishana maazo baada ya kumalizika hafla hiyo.

 


Baadhi ya pikipiki kati ya 300 ambazo watapatiwa maafisa ugani wa wizara hiyo.

 

Wakiwa na nyuso za furaha baada ya kumalizika  hafla hiyo toka kushoto ni Naibu waziri Abdallah Ulega, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka na waziri Mashimba Ndaki.

 


Na Mbaraka Kambona, Dodoma

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amekabidhi Pikipiki Mia Tatu (300) kwa Wakuu wa Mikoa 25 ili zikatumiwe na Maafisa Ugani wa sekta ya mifugo waliopo katika Halmashauri kwa lengo la kuwarahisishia kazi ya kuwahudumia wafugaji nchini.

 

Mhe. Dkt. Mpango alikabidhi pikipiki hizo muda mfupi baada ya kufungua Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma kuanzia Januari 17-18, 2022.

 

Wakati akikabidhi pikipiki hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Athony Mtaka kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wengine, Dkt. Mpango  alisema kuwa sekta ya mifugo ni moja kati ya sekta za kipaumbele kwa serikali, na ugawaji wa pikipiki hizo kwa maafisa hao ni katika jitihada za serikali kuboresha sekta hiyo ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa.

 

“Serikali inatambua changamoto za sekta hii, napenda kuwahakikishia serikali inaendelea kuzitatua na ndio maana leo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kununuliwa kwa pikipiki hizi, na tutaendelea kuboresha huduma za ugani ikiwemo kuendelea kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji wetu,” alisema Dkt. Mpango.

 

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Manispaa kutenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maafisa ugani katika maeneo yao huku akiwataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanazitumia vyema pikipiki hizo ili kuwasaidia wafugaji kufanya ufugaji wenye tija.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema pamoja na kazi kubwa inayofanyika ya kuboresha sekta hiyo ya mifugo, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya maafisa ugani na hivyo alimuomba Makamu wa Rais kuona uwezekano wa serikali kutoa kibali cha ajira kwa ajili ya maafisa ugani.

 

“Mhe. Makamu wa Rais pamoja na uwepo wa teknolojia ya ugani kiganjani, haiondoi uhitaji wa maafisa ugani, uhitaji ni mkubwa, tunaomba serikali iwaajiri maafisa hawa ili waje kusaidia wafugaji wetu huko waliko,”alisema Mhe. Ndaki.

 

Kuhusu pikipiki hizo, Mhe. Ndaki alisema serikali imetumia Shilingi Milioni 864 kununua pikipiki hizo na zitasambazwa kwa mikoa 25 na  Halmashauri 140 zinatarajiwa kufaidika na pikipiki hizo.

 

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa alisema kuwa ili kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kuleta tija kwa wafugaji watahakikisha asilimia 15 inayotakiwa kutengwa na Halmashauri kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo inatengwa na kusimamiwa vizuri zitumike kuendeleza sekta hiyo kama ilivyokusudiwa.

 

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda alisema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuandaa mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma za ugani wa wafugaji ili sekta ya mifugo iweze kuwa na tija zaidi nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages