HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 20, 2022

TUPO TAYARI KUMPOKEA CHIFU MKUU HANGAYA


Adeladius Makwega-Moshi

 

Machifu wa Mkoa Kilimanajro kwa pamoja wamesema kuwa maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la Kilimanjaro yamekamilika vizuri na wapo tayari kumpokea Mgeni Rasm Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan

 

Jeremia Senduia Laizer ambaye ni Olegwanani wa Wamasai wa Kilimanjaro amesema kuwa japokuwa jambo hili ni geni lakini muitikio umekuwa mkubwa sana.

 

“Hivi sasa sisi tupo tayari kumpokea Mkuu wetu wa Machifu Chifu Hangaya ambaye ndiye Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samiha Suluhu Hassan.”

 

Naye Chifu wa Wapare Gabriel Msofe alisema kuwa hata kwao wananchi wamehamasika mno kwani wametayarisha vikundi kadhaa vitakavyotumbuiza katika tukio hilo.

 

“Tumelichukua kwa uzito wa mkubwa Tamasha la Utamaduni la Kilimanjaro na ndugu zetu wa Upareni wanatamani kushiriki kuja katika tamasha hili lakini ni mbali na gharama ndiyo maana sisi na wenzetu kadhaa tutawakilisha vizuri.”

 

Wakiwa kandoni mwa kikao maalumu cha maandalizi chini ya Uenyekiti wa Chifu Mkuu wa Wachaga Frank Mareale, kwanza alisema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri huku akikumbusha historia ya uchifu nchini Tanzania.

 

“Hapo awali serikali ilipofuta uchifu, tulidhani ilifuta hadi utamaduni na jambo hili lilififisha mno mambo ya kimila laikini kumbe ilifuta mambo ya Uhakimu na Utawala tu lakini Utamaduni ulibaki na ndiyo maana tulirudisha Umoja wa Machifu nchini na ndiyo maana sasa tunaweza kufanya tamasha kama hili la utamaduni.”

 

Mwisho Chifu Mareale alisema kuwa mambo kadhaa ya kimila yatakuwepo katika tamasha hilo ikiwamo Ngesi, Mbege na Dengelua.

 

Tamasha Utamaduni la Kilimanjaro litafanyika Jumamosi ya januari 22, 2022 katika Viwanja vya Chuo Cha ushirika Moshi tangu saa moja ya asubuhi chini ya usimamizi wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages