Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila.
Na Mwandishi Wetu, Muleba
Wananchi waliovamia kwenye vitalu vya ranchi ya Kagoma watakiwa kuondoka kwa hiari katika eneo hilo kabla ya zoezi la kuwaondoa katika vitalu hilo halijaanza.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila ameeleza kuwa wananchi wote waliovamia vitalu vya wawekezaji waondoke kwa hiari yao kabla ya kuja kutolewa huku akifafanua kuwa kwa kitalu namba 10 na kitalu namba 1 kuna utaratibu uliowekwa baina ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ranchi ya Taifa (NARCO), Mkoa na kamati ya Usalama ya Wilaya ya Muleba na utaratibu huo upo wazi.
"Kuanzia leo Januari 3, 2022, watu wote waliovamia kwenye vitalu vilivyosalia, ukiondoa kitalu namba 1 na kitalu namba 10 kwenye ranchi ya Kagoma waondoke kwa hiari yao na baada ya tarehe hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa kwasababu watakuwa wameshindwa kutii amri halali ya Wilaya na Mkoa", ameeleza Mhe. Nguvila.
Ameeleza kuwa taarifa hii ni maamuzi ya Mkoa na Wilaya ya Muleba dhidi ya wavamizi kwenye ranchi ya Kagoma ndani ya eneo la Wilaya ya Muleba. Na maamuzi haya yametolewa kwa kuzingatia Sheria za Serikali za Mitaa kifungu cha 14 kipengele cha 2 na kifungu cha 15 kipengele cha 1 na cha pili ukurasa wa 97 Sheria ya mwaka 1997.
Ameongeza kuwa Sheria tajwa hapo juu imempa Mamlaka ya kusimamia na kuhakikisha Taratibu, Kanuni na Sheria zinafuatwa na watu wote ndani ya wilaya ya Muleba pia imempa mamlaka ya kutoa ufumbuzi wa mambo mbalimbali ili kutekeleza Sera ya Serikali za Mitaa ndani ya Wilaya ya Muleba .
Kwa kuzingatia Sera ya Uwekezaji katika ranchi, Serikali kupitia kampuni ya ranchi ya Taifa (Narco) imetenga maeneo ya Kagoma katika Wilaya ya Muleba na kutoa vibali vya kuendesha shughuli hiyo ya uwekezaji kwa mujibu wa Sheria namba 17 ya mwaka 2003 na kupitia vibali hivyo wamiliki wa vitalu wana haki ya kufanya shughuli zao kama masharti ya leseni zao yanavyoelekeza bila kubughudhiwa na mtu yoyote .
Ameendelea kueleza kuwa hivi karibuni kumetokea watu wachache wenye nia ovu, kuvamia maeneo ya ranchi ya Kagoma na kufanya uharibifu wa mali, kujeruhi watu na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hivyo basi ili amani na utulivu viendelee kuwepo watu waliovamia maeneo hayo wanatakiwa kuondoka.
Aidha amesema kuwa ni marufuku mtu yoyote asiyehusika na usimamizi au uendeshaji wa lanchi ya Kagoma kuingia na kufanya shughuli zozote kinyume na malengo yaliyopangwa na Serikali kwani atakayekiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria.




No comments:
Post a Comment