HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 20, 2022

BALOZI MULAMULA AMLILIA KAKA YAKE, PADRE AELEZEA SIFA ZAKE IKIWEMO KUWALEA YATIMA NA WASIOJIWEZA






Waziri wa Mambo ya je na ushirikiano wa kimataifa balozi Liberata Mulamula akiongea na waombolezaji katika msiba wa marehemu kaka yake.
Watoto wa marehemu Balozi Edwin pamoja na mke wake wakishuhudia na kuaga mwili wa mpendwa wao.

 

Na Lydia Lugakila, Misenyi

Vilio na majonzi vyatawala wakati mamia ya watu wakijitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Diplomasia ya uchumi wizara ya mambo ya nje Balozi Edwin Rutageruka ambaye amepumzishwa katika nyumba yake ya milele kijijini kwao Kitobo wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Marehemu  Balozi Rutageruka amefariki dunia Februari 13, 2022 katika hospitali ya Aga khan jijini Dar es salaam na mwili wake kuangwa Februari 19,2022 nyumbani kwao kitongoji cha Msibuka kata Kitobo wilaya ya Misenyi.

Akitoa neno katika ibada ya kuagwa kwa mwili wa balozi Edwin Rutageruka Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni dada wa marehemu Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa yeye kama upande wa wizara na kama mwanafamilia wamepokea kwa masikitiko makubwa kufuatia kifo cha marehemu Rutageruka.

Balozi Mulamula amesema akiwa katika ziara ya kikazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe, Samia Suruhu Hassan nchini Ufaransa alipokea taarifa za msiba huo kutoka kwa mmoja wa wanafamilia ambapo baada ya kumweleza Rais  taarifa hizo alimruhusu kurudi hapa nchini ili kuendelea na taratibu za msiba.


"Ilikuwa ghafla haikunijia kama ni kifo nashukuru wizara yangu iliyosimama bega kwa bega juu ya msiba huu, familia tumempoteza kitinda mimba wetu" alisema waziri Mulamula.

Akiongoza  misa takatifu Baba Paroko wa Parokia ya Bugango kutoka kanisa katoliki Padre Solomon Bandiho amesema kuwa maisha aliyoyaishi marehemu balozi Edwin ni zawadi toka kwa Mungu kwani amekuwa na upendo uliotukuka alimpenda sana Mungu na kanisa lake,familia yake, watoto yatima na wasiojiweza na waliojiweza hivyo itoshe kwa kila mtu kujiandalia mahusiano mazuri  ya badae kwa kujiweka tayari kwa kutenda mema ili siku ikifika waliobaki wakuseme mema

" Marehemu Edwin ameondoka amefanya makubwa ambapo hatosaulika kwa uchangiaji wa kigango Cha mtakatifu Theresia msibuka kwa asilimia 70, kuanzisha kampeini ya ONDOA NYASI na kuhakikisha waumini  katika kigango cha Msibuka wanakaa kwenye mabenchi badala ya kukalia nyasi hivyo tunapomsindikiza mwenzetu tujue utajiri tunaojikusanyia tukiwa duniani ni upendo na mahusiano mema kwa jamii, tukiwa hai "amesema Padre Bandiho.

Padre Bandiho ameongeza kuwa, marehemu Edwin Rutageruka alijitoa kuwalea vijana wa mijini na vijijini kwa kuwagharimia katika masomo vile vile alishiriki sana kuwasaidia wanandoa ambao hawakufunga ndoa waweze kubariki ndoa zao pamoja na kujenga makanisa Dar es salaam Mwanza na Bukoba.

Akisoma wasifu wa marehemu mtoto wa marehemu Brayn amesema kuwa marehemu balozi Edwin alizaliwa Oktoba 1965 katika Kijiji cha Msibuka Kata Kitobo wilayani Misenyi mkoani Kagera ameacha watoto 5  ambao ni Linda, Laura, Brayn, Cynthia na Desmond pamoja na mjane mmoja aitwaye Bi Kokuhumbya Kazaura.

Hata hivyo akitoa salamu za pole kwa niaba ya wizara Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Joseph Sokoine amesema kuwa wizara hiyo itaendelea kushirikiana na familia hiyo na kuwaomba waombolezaji na wanafamilia kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu

No comments:

Post a Comment

Pages