HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2022

Ewura bei ya dizeli imeongezeka shilingi 13 kwa lita


Kaimu Mkurugenzi Mkuu kutoka Mamlaka ya Udhibiti Wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje  akizungumza na waandishi wa habari hawapo (pichani) wakati akitoa mwenendo wa bei za mafuta nchini.

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa kuna uwezekano wa mkubwa wa kuongezeka kwa bei za  mafuta  mwezi Machi na Aprili mwaka huu.

Pia amesema bei za mafuta ya rejareja  mwezi Februari Petroli, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa shilingi 21  ya petroli na ya taa shilingi 44 kwa lita  wakati bei ya dizeli imeongezeka  kwa shilingi 13 kwa lita.

Ili kuhakikisha kunakuwa na ushindani sawa (Fair competition),katika bei zinazoanza kesho Februari 2, ununuaji wa mafuta kutoka kwenye maghala (Wholesale), sasa kutakuwa na bei mbili, bei kikomo ambayo muuzaji hatatakiwa kuzidisha na bei ya chini ambayo vile vile muuzaji hatakiwi kushuka zaidi.

Hayo ameyasema  jijini Dodoma leo wakati akitoa mwenendo wa bei za mafuta nchini amesema kuwa mamlaka hiyo itaendelea kufuatilia mwenendo huo kwa ukaribu ili kuishauri serikali hatua za kuchukua katika harakati za kupunguza makali ya  bei za mafuta.

Mhandisi Chibulunje amefafanua kuwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kaskazini Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimepungua kwa shilingi 123 Petroli, 92 dizeli kwa lita.

"Kutokana na kumalizika kwa mafuta ya taa kwenye maghala ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikao ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka Bandari ya Dar es Salaam," amesema.

Ameongeza kuwa bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta hayo kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji hadi katika mikoa hiyo.

Mhandisi Chibulunje ameeleza bei za rejareja za mafuata ya petroli dizeli kwa mikoa ya Kusini Mtwara, Lindi na Ruvuma zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Januari 5, mwaka huu.

" Hii ni kwa sababu kwa mwezi Januari mwaka huu hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara," ameeleza.

Aidha amewashauri waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa hiyo kuchukua mafuta ya taa  kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages