HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2022

Mavunde atamani kilimo kiwanufaishe wakulima kwanza


 

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema anatamani kuwaona wakulima nchini wakinufaika kwa kazi wanayoifanya.

Mavunde amesema hayo leo Jumamosi Februari 12, Muheza mkoani Tanga ambako yuko katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuhusu zao la mkonge ambalo ni zao la kimkakati linalolimwa mkoani hapa.

Mavunde amesema serikali ina malengo ya kukuza uchumi wa kaya na uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia zao la mkonge.

"Moja ya malengo ambayo serikali tumejiwekea ni kulipa kipaumbele zao la mkonge ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati na tutahakikisha tunaisaidia Bodi ya Mkonge kutimiza wajibu wake ili uzalishaji uongezeke mkulima anufaike na zao la mkonge.

"Nitoe rai kwa wananchi Mkoa wa Tanga na maeneo yote yanayolima mkonge nchini, niwaombe muendelee kuiamini bodi yetu na kufanya nayo kazi na mjitokeze kwa wingi sana kwenye kilimo hiki, najua mlikuwa na changamoto nyingi sana mkonge mwingi ulikuwa unabaki shambani hauvunwi kwa sababu ya uwepo wa makorona mengi ya kusaidia uvunwaji wa mkonge.

"Serikali tumedhamiria katika bajeti inayokuja na nimeshamuelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge kuanza mchakato mara moja wa kutangaza zabuni ya kununua makorona mengine matatu kwa ajili ya kusaidia uchakataji wa zao la mkonge ili pia tuwe tumerahisisha kwa wakulima kupata sehemu ya uhakika ya uchatwaji wa mazao yao," amesema Mavunde.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Saddy Kambona amesema amepokea maelekezo ya Naibu Waziri na kuongeza ni hatua kubwa mbele katika kuchochea uzalishaji wa kilimo cha mkonge.

"Sisi bodi tutahakikisha mchakato huu unakwenda haraka makorona haya yaweze kununuliwa haraka zaidi. Kwa hiyo niwatie shime wananchi kuendelea kulima mkonge serikali iko pamoja nao," amesema.

Akiwa ziarani Tanga, Mavunde ametembelea Jengo la Ofisi za Bodi ya Mkonge Tanzania, kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mkonge ambacho kinamilikiwa na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) na kusimamiwa na Kampuni Tanzu ya Sisalana, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na kuzungumza na wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos), vinavyolima mkonge mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment

Pages