HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 17, 2022

Mvua za kutosha zatarajiwa masika

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utabiri wa msimu wa masika ofisini kwake leo Februari 17,2022.
 

Na Irene Mark

MAMLAKA  ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetahadharisha kuwepo kwa  mvua kubwa za wastani mpaka juu ya wastani msimu wa Masika utakaoanza wiki ya pili ya Machi hadi mwishoni mwa Mei, 2022.

Mvua za Masika zitanyesha kwenye mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Mkurugenzi wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, amesema hayo leo Februari 17,2022 alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema utabiri wa msimu wa masika mwaka huu unaonesha kuwepo kwa mvua za kutosha sana kwenye mikoa yote inayopata mvua hizo huku akitaka sekta mbalimbali kuchukua hatua kudhibiti mvua hizo.

"...Mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwepo kwa mvua kubwa katika msimu wa masika unaonza Machi, Aprili hadi Mei na zitaanza kunyesha wiki ya tatu na ya nne ya Februari na kumalizika  mwishoni mwa Mei.

“Mikoa itakayopata mvua hizo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Kanda ya ziwa mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Mara na Shinyanga, Tanga, Dar es Salaam baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Pwani vikiwemo visiwa vya Mafia na Zanzibar.

“Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani mpaka juu ya wastani ambapo zinaweza zikaambatana na athari mbalimbali hivyo basi tunaziomba mamlaka husika za kudhibiti maafa kuchukua hatua kabla athari hazijatokea,” alisema Dk. Kijazi.

Kwa mujibu wa Dk. Kijazi, TMA ikishirikiana na wadau mbalimbali walikutana Februari 11,2022 na kuwashauri namna bora ya kupanga shughuli zao kwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa.

ATHARI
Amesema mvua hizo zinaweza kuleta athari kwenye sekta ya kilimo, miundombinu na usafirishaji.

“Kwa sababu ya mvua hizo, kunatarajiwa kuwepo na unyevunyevu mwingi kwenye udogo hali inayoweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko kwa baadhi ya maeneo.

“Aidha tunazitaka mamlaka kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kutokea kipindi cha mvua,” amesema Dk. Kijazi.

Ametumia fursa hiyo kuwaonya wachimbaji wa madini kutokana na ongezeko la maji katika udongo, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha ya binaadam.

FAIDA
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mvua za kutosha wakati huu wa masika zitasaidia kuondoa ugomvi wa malisho na maji ya mifugo kati ya wakulima na wafugaji.

Kuhusu kilimo amewashauri wakulima kuandaa mashamba na kupanda mbegu mapema kwa kutumia  mbinu bora za teknolojia kuzuia maji kutuama shambani.

Ameongeza pia sekta ya nishati itaboreka hasa kwenye nishati inayotegemea zaidi vyanzo vya maji huku akisisitiza wadau na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa kuzingatia zaidi taarifa za kila wiki na saa24 zinazotolewa na TMA.

Hata hivyo amesema katika mifumo ya hali ya hewa joto la bahari linatarajiwa kuwa la wastani hadi chini ya wastani katika Bahari ya Pasifiki na wastani kwenye Bahari ya Hindi.

Hata hivyo mvua za Masika zinaweza kuleta faida kwenye sekta ya kishati kwa kuongezeka kina cha maji wenye mabwawa lakini pia kwa wakulima Kwa wale watakaolima mazao yanaostahimili mvua nyingi kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa mazao.


Aidha pia kwa baadhi ya maeneo yanaweza yakakumbwa na mafuriko yatakayotokana na mvua hizi. Sekta ya madini, wachimbaji wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na mvua hizo ambazo zinaweza zikasababisha maporomoko ya udongo kwenye machimbo.


"Kiujumla tunashauri wananchi kufuatilia ushauri na maagizo yatakayotolewa na Mamlaka husika, TMA tutaendelea kufuatilia hali ya hewa na kutoa taarifa sahihi Kwa wananchi kupitia vyombo vya habari," alisema DK Kijazi.


Kufuatia utabiri huo, baadhi ya mikoa tayari imeanza kujipanga kuchukua tahadhari kukabiliana na athari zozote zinazoweza kutokea.


Akizungumza na Habari Mseto Katibu tawala wa Mkoa wa Kagera ambao unatarajiwa kuwa na mvua kubwa, Profesa Faustine Kamuzora, alisema wataanza kujipanga kukabiliana na athari zozote zinazoweza kutokea.


Alisema kuwa watachukua tahadhari zote kutokana na taarifa ya TMA ili kuhakikisha mkoa huo inakuwa salama na kufaidika na mvua zinazotarajiwa.


Katika utabiri wa mvua zikizopita (Vuli) TMA ilitabiri kuwepo Kwa auhaba wa mvua hali ambayo umepelekea kuwepo Kwa matukio ya ukame Kwa baadhi ya maeneo yanayopata mvua hizo pamoja na vifo vya mifugo kutokana na ukosefu wa malisho.

No comments:

Post a Comment

Pages