HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 16, 2022

RC Malima atoa maagizo matumizi kamba za plastiki


Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amewataka watengenezaji wa kamba za plastiki kujisalimisha na kuanza kulipia kodi za bidhaa hizo kabla hazijapigwa marufuku.

Aidha, amewataka wakazi mkoani Tanga kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa zinazotokana na mkonge zikiwamo kamba za katani ili kulinda na kukuza soko la mkonge na kutunza mazingira.

Malima amesema hayo leo Jumatano Februari 15, alipokutana na kuzungumza na uongozi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), walipokwenda kumtembelea ofisini kwake katika ziara yao ya kufanya uchunguzi wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu uingizwaji wa bidhaa zinazosababisha uchafuzi mazingira mkoani hapa.

Amesema katika uchunguzi uliofanywa kwa wauzaji wa kamba za plasitiki imegundulika hawajui zinapotoka kwa maana hiyo zinatengenezwa na viwanda bubu ambavyo havijulikani na havilipi tozo wala kodi.

“Mkoa wa Tanga tunataka kubaini hizo kamba zinatoka wapi ili tuwabane kwanza walipe kodi na kuwe na tozo itakayowezesha kupata fedha ya kutunza mazingira hayo wanayoharibu kwa mujibu wa sheria za halmashauri.

“Hizi kamba hazina majina ya kiwanda wala anuani na haisemi imetengenezwa wapi, hakuna mtu anataka bidhaa zake zisijulikane, kwa hiyo kiwanda hakijulikani lakini bidhaa sokoni zipo.

“Lakini pia tunataka kujenga utamaduni wa watu kutumia mkonge badala ya plastiki ili kuhamasisha matumizi ya bidhaa zitokanazo na mkonge kwa sababu kamba hizo zipo za kutosha viwandani.

“Suala la kwamba viwanda vyetu havina kamba za kutosha iwapo kamba za plastiki zitaondoka si kweli, Sisalana wana kamba hata hawajui wazipeleke wapi, tuna soko la kutosha. Lakini tunavyotoa msisitizo wa matumizi ya kamba za katani lazima nao waongeze uzalishaji siyo wabweteke,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC, Romanus Tairo wakiwa mkoani hapa wamekutana na wadau mbalimbali wa mkonge ikiwamo Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Chama cha Wakulima wa Mkonge nchini (SAT) na wadau wengine wa zao hilo na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu utunzaji wa mkonge na mazingira.

No comments:

Post a Comment

Pages