HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 16, 2022

SERIKALI KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI NCHINI


Na Hamida Ramadhani, Dodoma

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt Juma Maliki Akil amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi katika Mapambano dhidi ya Rushwa na Ubadhirifu (Ufisadi) Nchini.

 Amesema mbali na Jitihada za serikali za kuweka mifumo mbalimbali ya udhibiti lakini pia itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo PERTERMS Consultancy Ltd  katika kupambana na vitendo hivyo vya Ufisadi ambavyo wahalifu wanabuni njia mpya kila kukicha.

Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo jiji Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo ya siku tano juu ya “Kudhibiti Rushwa na Ubadhirifu katika Sekta ya Umma” yaliyo ratibiwa na Taasisi Patems Consultancy ya Jijini Dar es Salaam.

 “Rasilimani fedha inatakiwa kusimamiwa kwa umakini na ukaribu zaidi kwenye hatua zote ambazo ni Upatikanaji wake, Chanzo chake na mwisho Matumizi yake.

Amesema kumekuwa na matatizo katika suala zima la usimamizi wa fedha za Umma hususani upande wa matumizi ambako matumizi ya mashaka yamekuwa yakibainika mara kwa mara kama taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionyesha

" Ninaimani kupitia nyinyi Washiriki wa Mafunzo haya kwamba Ubadhirihifu wa mali za Umma utadhibitiwa katikaymaeneo ya kazi na hivyo kuleta mabadiliko katika tasinia ya mapambano dhidi ya Ufisadi kwa Imani kwamba elimu mlioipata italeta mabadiliko chanya kwenye maeneo yenu na hivyo kuongeza thamani na umuhimu wa mafunzo haya.

Katibu Mkuu aliongeza "Tija ya Mafunzo haitafikiwa ikiwa nikupata vyeti tu bali mlichojifunza mkafanye kwa vitendo msikiache kwenye makaratasi" amesema .

Naye CFE Shakibu Mussa Nsekela ambae ni Bingwa katika masuala ya kudhibiti Rushwa na Ubadhirifu amesema mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono jitihada za Serikali katika Mapambano dhidi ya Ufisadi kwani mapambano haya ni yetu sote na kila mmoja wetu anao wajibu wa kuhakikisha taratibu na kanuni zinazingatiwa katika utendaji kazi wetu wa kila siku hususani katika kusimamia rasilimali za Taifa.

" Inaaminika kwamba kila Sekta inazo changamoto zake kwa watumishi hasa pale wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. Baadhi ya changamoto hizo ni kutishiwa ajira, kushushwa vyeo nk, lakini Pamoja na changamoto hizo, lazima kila mmoja wetu atekeleze majukum yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu husika huku akiongozwa na maadili ya Taaluma yake (Professionalism)," amesema


Na kuongeza "Mafunzo haya ni muhimu hususani kipindi hiki ambacho Serikali Imedhamiria kwa vitendo kuhakikisha kila Mtanzania anatimiza wajibu wake katika ujenzi wa Uchumi wa Nchi kwa ajili ya maendeleo kwa kuhakikisha rasilimali za taifa hili zinatumika kwa usahihi na kama ilivyokusudiwa ili kuleta faida kwa vizazi vya sasa na baadae," Mtaalam huyo.

Pia CFE Nsekela amezishauri Taasisi zote bila kujali Sekta kwamba ili kudhibiti vitendo vya ufisadi, lazima Taasisi hizo zihakikishe zinazingatia weledi, kuajiri watu sifa na maadili sahihi, mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi, mifumo sahihi ya udhibiti na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika kuna uhalifu katika rasilimali za Umma.

Akiongea kwaniaba ya washiriki wanzake, Mshiriki Dr Rose Ntundu kutoka NHIF Ameeleza kuwa mafunzo ya aina hii ni muhimu sana kwa watumishi wa sekta zote za Umma na Binafsi kwani Mbali na kubadilishana uzoefu lakini washiriki wameweza kujifunza mbinu mbali mbali za kukabiliana na ufisadi kwenye maeneo yao ya kazi kwani wahalifu wanabuni njia mpya kila siku na hivyo bila mafunzo ya aina hii kuwepo mara kwa mara, wahalifu wanaweza kuendeleza uhalifu wao kirahisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mtendaji wa Patems Consultancy Ltd ambayo ni Taasisi iliyoanzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuongeza kazi ya mapambano dhidi ya Ufisadi CPA Charles Masolwa (Kamishna Msaidizi Mstaafu – FIU), amesema wao wamekusudia kuendelea kuunga Mkono jitihadi za Serikali katika kupambana na Vitendo vya ufisadi kwa kuhakikisha watoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wa sekta zote, lakini pia kufanya ukaguzi (Fraud Examination) kwa Makampuni na Taasisi zenye uhitaji ili kusaidia kubaini, chanzo, hasara na wahusika lakini pia kuzishauri taasisi hatua muafaka za kuchukua ili kudhibiti uhalifu kama huo usiendelee

Kamishna Masolwa, amesema kuwa Rushwa na Ubadhirifu ni uhalifu unaoweza kufanywa na Mtu wa ngazi yeyote wakati wowote na mahala popote, hivyo akashauri kuwa ili kushinda mapambano haya, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha sheria taratibu na kanuni zinazingatiwa wakati wowote na kwa ngazi yeyote katika usimamizi wa mali za Umma.

 Ameendelea kusema tafiti zinaonyesha kuwa kinga dhidi ya ufisadi kutokea ni bora kuliko kutibu na mafunzo  ya mara kwa mara kwa watumishi ni njia inayopendekezwa na waliowengi "Nia yetu ni taasisi ziweke mazingira ya kuzuia kwa uhalifu wa aina hii mapema, na pale inapotea uhalifu huu ukafanyika mifumo husika iweze kubaini na  hatua stahiki kuchukuliwa bila kuonea au kujali cheo cha Mhusika wa uhalifu huo (Mbadhirifu).

No comments:

Post a Comment

Pages