HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 08, 2022

TRC yasaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa 1430 na CRRC International

Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa (kulia) pamoja na Kaimu Meneja wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Reng (kushoto) wakisaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa 1430 kwa ajili ya Reli ya Kisasa.

 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ununuzi wa Mabehewa 1430 ya mizigo kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya CRRC International kutoka nchini China unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 127.2 kwa ajili ya reli ya kisasa SGR.

 Mkataba huo ni wa ununuzi wa mabehewa hayo ya mizigo za reli hiyo – SGR ambao, ni wa miezi 12 mwaka mmoja utakaohusisha usanifu na utengenezaji wa Behewa kwa ajili ya kubeba mizigo ya aina mbalimbali kulingana na aina ya behewa na matakwa ya mteja kupitia reli ya kisasa.

Akizungumza katika Hafla ya utiaji saini mkataba huo leo jijini Dar es salaam Waziri huyo Prof. Mbarawa amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha huduma ya usafiri wa mizigo inaimarika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kuongeza pato la taifa na kukuza uchumi.

"Ujenzi wa Reli ya kisasa unaoendelea hivi sasa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho kimefika 95%, Morogoro – Makutupora ambacho kimefika 81% na kipande cha Mwanza – Isaka ambacho kimefika 4% ni ishara tosha kwamba Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuongeza ufanisi na kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji kupitia reli,"amesema Waziri Prof Mbarawa.

Amebainisha kuwa kutokana na uwezo mkubwa wa reli ya kisasa mabehewa hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo treni moja itakuwa na uwezo wa kubeba Tani 10,000 kwa mkupuo ambayo ni sawa na malori 500.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa amezitaja aina za behewa zitakazonunuliwa kupitia mkataba huo kuwa ni pamoja na Behewa 600 aina CCB kwa ajili ya kubeba makasha, Behewa 400 aina ya CLB  ili kubeba mizigo ya jumla ikiwemo Sukari, Saruji, Chumvi, Pamba, Tumbaku na Kahawa, Behewa 190 aina ya PTB kubeba mafuta aina zote,na Behewa 70 aina ya HLB kwaajili ya Mabomba, Mbao, Magogo na Vyuma, Behewa 50 aina ya MGB kwaajili ya kubeba magari na Behewa 50 aina ya CWB (Cattle Wagon Bogie) kwaajili ya kubeba Ng’ombe.

‘Mkataba huu ni miongoni wa mikataba kadhaa ambayo TRC imesaini kwa ajili ya manunuzi ya vichwa na behewa za abiria na mizigo kwaajili ya shughuli za uendeshaji wa reli ya kisasa. Shirika limesaini Mkataba na Kampuni ya EUROWAGON ya Uturuki tarehe 1 Oktoba, 2020 kwa ajili ya ununuzi wa vichwa viwili (2) vya treni ya umeme na behewa 30 za abiria. Mkataba huu una thamani ya EURO milioni 26.60. Mkandarasi anatarajiwa kuleta vifaa hivyo mwezi Aprili, 2022’amesema Kadogosa

Amefafanua kuwa kitaalamu ili kuzalisha faida katika biashara ya usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya kisasa itahitaji angalau kusafirisha mizigo kwa umbali usiopungua KM 500, hivyo wanatarajia kwamba kukamilika kwa manunuzi na kuwasili kwa behewa hizo mapema mwaka Februari 2023 kutakwenda sambamba na kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Morogoro – Makutupora ambapo kwa umbali huo huduma ya usafirishaji mizigo itaweza kuleta tija kwa taifa.

Nae,  Kaimu Meneja wa Kampuni ya CRRC International Tang Yun Reng amesema wataendelea kushirikiana na TRC ili kuweza kukamilisha kwa wakati huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Prof. John Kondoro ameeleza maendeleo ya ujenzi wa mradi huo kuwa unaendelea.

 Hata hivyo wasimamizi wa TRC kuendelea kuchapa kazi kwa kutumia weledi walionao na jitihada ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuhudumia wananchi kwa miradi inayoendelea kukamilika kwa wakati.



No comments:

Post a Comment

Pages