Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Jerry Slaa (Mb), akielekeza jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ludovick Nduhiye (wa pili kushoto), wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri haraka wa mabasi (BRT) awamu ya pili, unaotekelezwa mkoani Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri haraka wa mabasi awamu ya pili, mkoani Dar es Salaam unaotekelezwa na Kampuni ya SINOHYDRO Corporation Ltd kutoka China.
Akiongea na waandishi wa habari katika eneo la BP lililopo kwenye barabara ya Bandari Mwenyekiti wa kamati hiyo Jerry Slaa ambae pia ni Mbunge wa jimbo la Ukonga ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri haraka wa mabasi (BRT) mkoani Dar es Salaam, ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba.
“Wakandarasi hawa wanalipwa fedha za watanzania iwe za ndani au za nje, hivyo ni vyema wakilipwa wafanye kazi ya kiwango na kwa kuzingatia muda ulioainishwa kwenye mkataba, ili fedha zilizowekezwa ziweze kuleta tija na kuifanya Dar es Salaam kuwa mji wa kisasa,” amesema Slaa.
Ameongeza kuwa ni vyema TANROADS ikamsimamia kwa karibu Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika ndani ya muda uliokusudiwa, kwani kukamilika kwa mradi huo kutawezesha wakazi wa mkoa wa Dar es salaam hasa waishio maeneo ya Mbagala kusafiri kwa haraka zaidi tofauti na ilivyo sasa na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Ludovick Nduhiye, amesema kuwa Wizara yake inaendelea kuisimamia TANROADS na kwamba katika mradi huo, kazi za ujenzi wa barabara, daraja la waenda kwa miguu, barabara za juu, daraja moja la juu ya reli pamoja na vituo vya mabasi zimefikia asilimia 50.7, na kwamba kwa mujibu wa mkataba mradi huu unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Machi, 2023. Aidha, ujenzi wa karakana, vituo vikuu viwili na vituo vya mlisho vinne tayari umekamilika.
Awali akisoma taarifa yake mbele ya kamati hiyo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema kuwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri haraka wa mabasi awamu ya pili unahusisha barabara za Kilwa, kutoka makutano ya barabara ya Bandari, barabara ya Bandari - Gerezani (Kariakoo), Barabara ya Chang’ombe kutoka makutano ya barabara ya Nyerere hadi Mgulani, barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Barabara ya Nyerere na barabara ya Sokoine kutoka Gerezani hadi Jengo la Mwalimu Nyerere.
Amefafanua kuwa ndani ya mradi huo wa awamu ya pili, kuna ujenzi wa barabara Kilometa 20.3, barabara za juu (flyovers) mbili, daraja moja la juu la waenda kwa miguu katika eneo la Mbagala, daraja moja la juu ya reli katika eneo la BP kwenye barabara ya Bandari hadi Gerezani, karakana moja ya mabasi, vituo vikuu vya mabasi (terminals) viwili, vituo vya mabasi (stations) 27, na vituo vya mlisho (feeder stations) vinne.
Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wameitaka TANROADS kuwasimamia kwa karibu wakandarasi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wakandarasi wanaochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo ili fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi hiyo itumike kuleta tija kwa taifa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment