Na Dotto Mwaibale, Singida
MADEREVA sugu wanne wa mabasi makubwa ya abiria wamekamatwa mkoani Singida na kuwekwa mahabusu tayari kwa kupelekwa mahakamani kesho kutwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa wakati akizungumza na madereva, wananchi na wasafiri kwenye opareshesheni maalumu ya kukagua mabasi ya masafa marefu iliyofanywa na jeshi hilo Stendi Kuu ya Mabasi mkoani hapa jana.
Alisema madereva hao waliokamatwa wamekuwasugu kwani wameonywa mara kadhaa, kulipishwa faini kupewa elimu lakini wameshindwa kubadilika ndio maana wamekamatwa na kuwekwa mahabusu na kesho kutwa watapelekwa mahakamani.
Alisema katika oparesheni hiyo magari yaliyokaguliwa ni mabasi 63, waliolipishwa faini ni madereva 16 na wale madereva sugu walikuwa wanne ambayo ametaja namba za mabasi waliokuwa wanayaendesha kuwa ni T 612 CQB la Kampuni ya ALPHA, T732 DTK la Kampuni ya Masalu, T 349 DUB la Kampuni ya Nyhaunge na T 684 DGW la Kampuni ya Simiyu Dream Line.
Alisema katika oparesheni hiyo pia wameweza kuwabaini madereva 40 ambao wanazingatia sheria zote za usalama barabarani ambapo aliwataka madereva wengine kuiga mfano huo.
Mutafungwa aliwataja madereva wengine waliowakamata kuwa ni wale ambao mabasi yao mfumo wa kubaini mwendo ulikuwa hausomeki ambao idadi yao ni watatu na wamewakabidhi Mamlaka ya Uthibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA ) kwa hatua zaidi.
Alisema kazi ya kwanza walioifanya katika oparesheni hiyo ni kutoa elimu kwa abiria na madereva kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ili kulifanya eneo la barabarani kuwa salama na kuwa eneo la kwanza ilikuwa ni kutoa elimu kwa makundi yote yanayotumia barabara.
Alitaja kazi nyingine walioifanya ni kukagua miendendo ya mabasi hayo yanaposafiri kutoka eneo moja kwenda lingine na kuangalia makosa mbalimbali ya usalama barabarani hasa makosa hatarishi ambayo yanagharimu maisha ya watu na mali zao.
Mutafungwa aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni mwendokasi na kuyapita magari mengine bila ya kuzingatia usalama na sheria ambayo wamekuwa wakiyabaini kupitia mifumo yao mbalimbali walionayo ukiwemo wa VTS na madereva ambao wanawabaini kwa makosa hayo wamekuwa wakiwachukulia hatua.
Wakati huo huo Mutafungwa aliwaomba wananchi wanaposafari wakikuta mabasi hayana mikanda ya usalama wasiyapande kwa ajili ya usalama wao na kueleza kwamba uhai wa binadamu haununuliwi hivyo wanapaswa kuzingatia jambo hilo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa alisema oparesheni mbalimbali zinazofanywa mara kwa mara na jeshi hilo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment