Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), linatarajia kuwekeza Sh. bilioni 13 kwaajili ya teknolojia ya kijani katika kilimo cha Mtama, Maharage na Alizeti.
Fedha hizo zitatumika kwenye awamu ya pili ya mpango wa kilimo himilivu kinacholenga kuwapa wakulima wadogo ujuzi huo na kupata mazao mengi yaliyo bora.
Mpango huo utakaoanza Julai mwaka huu, ni miongoni mwa vipengele vinane katika Mpango mkakati wa pili wa WFP wa mwaka 2022 mpaka mwaka 2027 utakaohusisha mikoa ya Dodoma, Manyara, Singida, Arusha, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Mara.
Mkuu wa ofisi ndogo ya WFP jijini Dodoma, Neema Sitta alisema mradi huo wa awamu ya pili ni matokeo chanya ya mradi wa kwanza unaomalizika Juni mwaka huu ambao nao ulikuwa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2017.
Neema alisema mradi huo pia kama ulivyokuwa wa awali umefadhiliwa na shirika la msaada la Ireland la IrishAid ambapo watakuwa wakitoa kiasi hicho kwa mwaka.
"Mpango huu utatekelezwa chini ya usimamizi wa WFP na kuratibiwa na FarmAfrica huku sisi (WFP) jukumu letu ni kusimamia programu katika ngazi ya wilaya na vijiji.
"WFP iliamua kupanua wigo kwenye mazao ya alizeti na maharage kwa sababu mahitaji yake yameongezeka katika siku za hivi karibuni.
“...Pamoja na hayo tunaunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania inayohimiza uwezeshaji wa wakulima wadogo wa alizeti na maharage,” alisema Neema.
Kwa mujibu wa Neema, mpango huo utazingatia usaidizi wa kibinadamu hasa kwa wakimbizi, udhibiti na upunguzaji wa hatari za majanga, mpango wa lishe kwa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na ulishaji chakula kwa wanafunzi wa shule za Msingi.
Vipengele vingine kwenye mpango huo ni kuimarisha ugavi kwa njia ya usindikaji na kuongeza thamani, usaidizi wa maisha kwa sekta mtambuka ambapo jamii zinajishughulisha na kuongeza kipato kama vile uvuvi, ufugaji na uhifadhi miongoni mwa mengine.
WFP pia itatumia mpango mkakati huo kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa serikali na sekta kibinafsi.
“Kilimo kinachozingatia hali ya hewa (Kilimo himilivu) katika awamu yake ya kwanza 2017/22 inayoishia Juni mwaka huu, kimewafikia wakulima 22,000 wa mtama kutoka wilaya sita za mkoa wa Dodoma ambazo ni Kongwa, Chemnba, Mpwapwa, Chamwino, Bahi na Kondoa.
“Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2021 tani 28,000 za mtama zenye thamani ya Sh. bilionj 13.5 zimeuzwa na wakulima kwa wanunuzi mbalimbali.
“Kwa hiyo idadi ya walengwa inatarajiwa kuongezeka maradufu katika awamu ya pili ukilinganisha na awamu ya kwanza,” alisema Neema.
Alisema licha ya kuwabadilishia wakulima modeli na mbinu za kisasa za kilimo, mpango huo unawazuia wakulima kukutana na 'mtu wa kati' katika uuzaji wa mazao yao ambapo sasa mkulima atakutana na mnunuzi bila kuwepo dalali.
Mradi huo tangu kuanza kwake awamu ya kwanza, kumeimarisha soko la mtama kwa wakulima ambapo kwa sasa thamani ya zao hilo imepanda kutoka Sh.200 hadi Sh. 250 kwa moja hadi Sh. 550 kwa kilo moja.
"Huko nyuma bei ilichangia watu kutolima zao hili kibiashara, bei ilikuwa chini sana ambapo walikuwa wakiuza kwa Sh. 250 ambapo hiyo ndio ilikuwa bei ya juu zaidi, lakini kwa sasa bei ni nzuri na inafanya wakulima wengi kujitokeza kulima zao la mtama kibiashara," alisema Neema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Wilaya ya Mpwampwa, Mwanahamisi Ali ambaye wilaya yake ni mmoja ya wilaya sita zinazotekeleza mradi wa awamu ya kwanza ya kilimo himilivu cha mtama.
"Kwa sasa hawa wenzetu wa WFP kwa kushirikiana na Serikali wameliinua sana soko la Mtama, bei ya sasa imechangia wananchi wengi kuingia kwenye kilimo cha zao hili kwa sababu kuna uhakika wa soko," alisema Mkuu wa Wilaya huyo.
Alisema kwa upande wao kama wilaya wataongeza chachu kwa wananchi kulima kwa wingi zao la mtama na mazao mengine kwa kuboresha maghala ya kuifadhia mazao hayo.
Alisema kutokana na uhaba wa mvua na hali ya ukame katika mkoa wa Dodoma mtama ni mkombozi wa wananchi.
Mbali na Kampuni ya bia Tanzania (TBL) na wanunuzi wakubwa kama Ali Juma kuongoza kununua mtama unaozalishwa kwenye mradi huo, bado mahitaji ya zao hilo katika soko ni mkubwa na haulingani na uzalishaji.
Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Farm Afrika, Grace Changamike, anasema nchi ya Sudan Kusini inahitaji mtama tani 10,000 kutoka Tanzania lakini pia kampuni ya bia ya Burundi inahitaji mtama kutoka Tanzania.
"Sasa ukiangalia kwa wanunuzi hao ambao wote wanahitaji maelfu ya tani za mtama unaona uhitaji ni mkubwa kulinganisha na uzalishaji, sisi kama wasimamizi wa mradi huu tutaendelea kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji hili kufikia mahitaji ya soko," alisema Grace.
Alisema awamu ya pili ya mradi huo utaongeza uzalishwaji wa zao la mtama na angalau kufikia mahitaji ya kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa wakulima wa zao la mtama aliyepata mafanikio makubwa kwenye awamu hii ya kwanza ya kilimo himilivu, Patrick Mbeo, kutoka katika kijiji cha Mnkola kata ya Ibhiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, alisema mradi huo umemuongezea mbinu ya kilimo hicho na kusababisha kulima ekari nyingi zaidi.
"Wakati nalima kama kilimo cha chakula zao hili la mtama nilikuwa nalima chini ya ekari moja, lakini tangu nimeanza kilimo cha biashara kupitia mradi huu nimekuwa nikiongeza ekari kwa sasa nalima zaidi ya ekari 20 na zimeniletea faida kubwa sana," alisema Mbeo.
Kauri hiyo inaungwa mkono ya mkewe, Happy Lukupe ambaye anasema mbali na kufanikiwa kununua mashine mbalimbali za kilimo ikiwemo mashine maalum ya 'kupula' mtama, wamefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa kijini hapo ambayo wanaitumia kwa biashara.
Mratibu wa mradi huo wilaya ya Mpwapwa, Adelina Ayoub alisema katika eneo lake kuna vikundi 95 vya wakulima na wakulima 5,079 wanajishughulisha na mpango huo.
Katika msimu uliopita, wakulima wa Mpwapwa peke yake walikuwa wameuza tani 13,077 za mtama kwa wanunuzi mbalimbali.
March 15, 2022
Home
Unlabelled
Teknolojia ya kijani kutumia Bil.13/- kilimo cha mtama, alizeti
Teknolojia ya kijani kutumia Bil.13/- kilimo cha mtama, alizeti
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.
No comments:
Post a Comment