Kaimu Meneja Rasilimali Watu wa Bandari Dar es Salaam, Mwajuma Mkonga akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo mfano wa kadi ya bima afya.
Na Selemani Msuya
WAFANYAKAZI
wanawake wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wamewalipia bima ya afya
watoto 400 kutoka wilaya za Temeke, Ilala na Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Wanawake hao
wametoa msaada huo uliolenga familia zenye maisha magumu, ikiwa ni
mwendelezo wa maadhimisho ya siku ya wanawake ambayo ilifanyika Machi 8
mwaka huu.
Akizungumza na
waandishi wa habari kabla ya kukabidhi bima hizo, Kaimu Meneja
Rasilimali Watu wa TPA Dar es Salaam, Mwajuma Mkonga alisema wamesukumwa
kusaidia watoto hao ikiwa ni sehemu ya wao kurudisha kidogo kwa jamii.
Mkonga
alisema wafanyakazi wanawake, mwajiri wao na wadau mbalimbali
wameshiriki kupata fedha ambazo zimeweza kulipia bima ya afya kwa watoto
400.
"Katika kuendeleza
maadhimisho ya siku ya wanawake sisi wanawake wa bandari tumechangishana
fedha kidogo ambazo zimeweza kulipia bima ya afya kwa watoto 400 wa
wilaya ya Temeke, Ilala na Kigamboni," alisema.
Kaimu
Meneja huyo alisema Wilaya ya Temeke wamelipia watoto 200, Ilala 100 na
Kigamboni 100, hivyo ni imani yao kuwa watoto hao watanufaika kwa
kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema
pamoja na kulipia bima kwa watoto hao wametembelea Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa ambovyo
vimegharimu Sh.milioni 5.
Alisema msaada huo ni sehemu ya wao kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kuresha huduma za afya.
Mkonga ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza na kusaidia jamii hasa yenye changamoto.
Naye
Mlezi wa watoto waliopatiwa bima hizo, Fatma Mohammed alisema msaada
huo utawasaidia kutatua changamoto ya matibabu kwa watoto anaowalea.
"Sijui
niseme nini, furaha niliyonayo haina kifani, ninachoweza kuwalipa ni
kumuomba Mungu awazidishie mlichotoa na mwakani mtoe tena. Mmetusaidia
pakubwa,"alisema.
Kwa
upande wake Kaimu Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Temeke, Emma
Komba aliwapongeza wanawake wa TPA kwa kuipa Temeke kipaumbele na kwamba
wamechagua sehemu sahihi.
Komba
alisema zoezi la kuwapata watoto wahitaji limeenda vizuri ila wanaomba
wadau wengine waendelee kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira
magumu kupata bima.
"Tunawashukuru
sana kwa msaada wenu kwani umeweza kusaidia familia zenye hali ngumu ya
maisha, zikiwemo familia za mapacha," alisema.
Komba alisema katika wanufaika wa bima hizo wapo pia wanafunzi kutoka Shule ya Msingi Mbagala na Sandali.
Akizungumza
baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo
alisema wanawake wa TPA wamefanya jambo kubwa ambalo linapaswa kuuungwa
mkono, huku akiwaomba na mwakani kuwakumbuka tena.
Mwegelo
alisema dhamira ya Serikali ni wananchi kupata huduma bora za afya
hivyo walichofanya wanawake wa TPA ni ushuhidi tosha wa kuunga mkono
juhudi za Serikali katika afya.
"Kusema
ukweli hili mlilofanya linapaswa kuigwa na kila mpenda maendeleo,
niwaombe mwakani tena mtukumbuke bado uhitaji ni mkubwa,"alisema.
Aidha,
Mwegelo aliwataka wazazi na walezi wa watoto hao kutumia fursa hiyo ya
bima ya afya kuongeza uzalishaji ili mwakani waweze kukata wenyewe.
Mkuu
huyo wa wilaya aliwataka wananchi wa Temeke kuhakikisha wanawachukulia
watoto wao vyeti vya kuzaliwa hali ambayo itaondoa usumbufu ambao
unajitokeza kwenye kukata bima ya afya.
No comments:
Post a Comment