Akizungumza
na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, katika mkutano maalum, Waziri
Simbachawene amesema Wizara yake imefanya mambo mengi katika kuwatumikia
Watanzania ambapo katika hayo ina maeneo yaliyofanikiwa zaidi.
“ Kwa upande wangu kama Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, nitazungumzia mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Sheria kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan”, amesema Waziri Simabachawene
Ameyataja maeneo hayo Waziri Simbachawene amesema Wizara inajivunia kuimarisha mfumo wa utoaji haki nchini kwa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili katika uandishi wa sheria na shughuli za utoaji haki mahakamani sambamba na kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro nje ya mahakama kwa kutumia njia ya majadiliano, maridhiano, upatanishi na usuluhishi.
“ Jambo lingine la mafanikio ndani ya huu mwaka mmoja ni uteuzi wa majaji tisa (9) wa Mahakama ya Rufani na Majaji 21 wa Mahakama Kuu na kufanya jumla ya idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kufikia 24 na Majaji wa Mahakama Kuu kufikia 82 na Mahakimu 245”,ameongeza.
Amebainisha kuwa kupitia mabadiliko ya sheria, wigo wa uwakilishi katika mfumo wa utoaji haki umeongezeka baada ya mawakili kuanza kutoa huduma za uwakili katika mahakama za mwanzo pamoja na kuanzishwa kwa vituo jumuishi vya utoaji haki vya mahakama katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Morogoro na Dodoma ili kuhakikisha utawala wa sheria na utoaji haki vinazingatiwa.
Masuala mengine ni pamoja na kuboreshwa na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za kimahakama kwa kukamilisha ujenzi wa majengo na kukarabati miundombinu mbalimbali ya Mahakama pamoja matumizi ya TEHAMA katika mfumo wa utoaji haki Kupunguza mlundikano wa mahabusu na kuongezeka kwa kiwango cha usikilizwaji wa mashauri katika Mahakama.
Ameongeza kuwa , kuongezeka kwa kiwango cha usajili wa matukio muhimu ya binadamu, kuunganishwa kwa mfumo wa wakala wa usajili, ufilisi na udhamini na mahakama ambapo imerahisisha uhakiki wa amri za Mahakama kupitia njia ya mtandao.
Waziri Simbachawene pia amesema Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi tano (5) kati ya nchi 54 za Afrika kuongoza katika ukanda wa Mashariki kwa kuwa mojawapo ya nchi yenye utashi wa kisiasa ni jambo la kujivunia katika kutekeleza kikamilifu kanuni zinazounga mkono kampeni ya kuongeza kasi ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu barani Afrika.
Kwa upande wa mawasiliano Tanzania imefanya vizuri kwa kutoa taarifa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na Ulimwengu kwa ujumla kuhusu jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha, kukuza, kuheshimu na kulinda haki za binadamu na watu.
No comments:
Post a Comment