HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 13, 2022

MRADI WA UJENZI SOKO LA MACHINGA COMPLEX DODOMA KUOKOA GHARAMA ZA WATUMISHI


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

Mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara ndogondogo (Machinga Complex) jijini Dodoma umesaidia kuokoa gharama za watumishi wa serikali wakiwemo, wakurugenzi, wakuu wa wilaya, makatibu tawala na wakuu wa wilaya kwenda nje ya nchi kujifunza utekelezaji wa miradi inayofanana na huo.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa wakati akizungumza kwenye mradi wa ujenzi wa Machinga Complex baada ya baadhi ya wakuu wa mikoa hapa nchini kutembelea mradi huo kwa ajili ya kujifunza.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema baada ya baadhi ya  wakuu hao wa mikoa pamoja na makatibu tawala kujifunza utekelezaji wa mradi huo itawasaidia kufanya miradi yenye ubora inayofanana na mazingira wanayotoka .

Hata hivyo,Waziri Bashungwa amewataka wakuu wa mikoa  na makatibu tawala kuwa wabunifu katika utekelezaji wa miradi inayokwendana  mazingira halisi ya watumiaji.

Nao baadhi ya wakuu wa mikoa  waliofika katika  soko la Machinga Complex wamesema watahakikisha wanajenga masoko ya viwango katika maeneo yao baada ya kujifunza muonekano wa soko  hilo.

Mkurugenzi wa kampuni ya MOHAMMED BUILDERS inayotekeleza mradi wa soko hilo, TAHER  JAFFERTI  ameupongeza mkoa wa Dodoma kwa kuwa imara katika usimamizi wa utekelezaji wa mradi huo huku mshauri mwelekezi wa mradi huo Dkt.Ibrahim Msuya akibainisha vigezo muhimu wa utekelezaji wa mradi wa soko hilo.

Miongoni mwa wakuu wa mikoa waliotembelea kujifunza katika soko la Machinga Compex  Dodoma ni kutoka mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Songwe, Morogoro, Iringa na Mwanza ambapo kati ya Tsh.Bilioni 5 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha miundombinu ya Machinga,Milioni 500 imeletwa utekelezaji wa soko la Machinga Complex huku ujenzi ukitarajiwa kukamilika mwezi Mei Mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages