- Ni kwa deni la Sh232 milioni za wanahabari
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mmiliki wa Kampuni ya makampuni ya Quality Group Limited, Yusuf Manji atakuwa amejiweka kwenye hatari ya kukamatwa endapo atashindwa kutokea mahakamani kueleza kwa nini ameshindwa kuwalipa Sh232 milioni waandishi wa habari waliokuwa wameajiriwa katika kampuni yake.
Jana, gazeti moja la kila siku limechapisha tangazo la kuwataka wawakilishi wa kampuni hiyo kufika Mahakama Kuu (Divisheni ya Kazi) Aprili 20, mwaka huu kueleza kwa nini wameshindwa kulipa kiasi hicho waandishi wa habari 23 waliowaachisha kazi katika gazeti la Jamboleo Septemba 19,2017.
Wafanyakazi hao wanadai pesa hizo kufuatia tuzo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Temeke, iliyotolewa Juni 24, 2019 baada ya kuiburuta kampuni hiyo katika tume hiyo kupinga kuachishwa kazi.
“Mnajulishwa kuwa shauri la maombi madogo tajwa hapo juu limepangwa kusikilizwa na mahakama hii Aprili, 2022 mbele ya E.M. Kassian, Naibu Msajili."
“Mnapaswa kuhudhuria siku na tarehe iliyopangwa bila kukosa na endapo hamtahudhuria nyinyi au wawakilishi wenu wanaotambulika kisheria, basi maombi hayo yatasikilizwa bila uwepo wenu,” linaeleza tangazo hilo.
Mwakilishi wa waandishi hao, Joseph Lugendo amesema tangu wapate tuzo hiyo wamekuwa wakiitaka kampuni hiyo iwalipe haki yao bila mafanikio.
Amesema wamefikia uamuzi wa kufungua maombi mahakamani kwa mara nyingine Manji akamatwe kwa kuwa ndiye aliyesaini barua za kusitisha ajira yao kinyume cha utaratibu.
Ameeleza kuwa kabla ya tangazo hilo, mahakama ilitoa hati ya kumuita Manji au wawakilishi wa kampuni yake Februari 24 mwaka huu, lakini wanasheria waliokuwa wakiiwakilisha kampuni hiyo na mmiliki wake walidai hawana tena mkataba na mteja wao huyo wa zamani.
Lugendo amesema baada ya kushindwa kumpata Manji wala wawakilishi wa kampuni hiyo, walirudi mahakamani Machi 29 mwaka huu, kuomba kutangaza wito huo gazetini ili wafike kortini kueleza sababu za kutolipa malipo hayo.
“Miongoni mwa waandishi ninaowawakilisha, wapo wanaodai zaidi ya Sh 3 milioni na wengine chini ya hapo. Hatuoni sababu za kampuni hiyo kushindwa kulipa madai yetu,” amesema Lugendo.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, hati ya kupinga kuondolewa kazini kwa waandishi hao iliwasilishwa kwa usuluhishi ambao ulishindikana na Oktoba 24, 2017, ilihamishiwa kwa ajili ya uamuzi.
Waandishi hao waliajiriwa katika kampuni hiyo katika nafasi mbalimbali kwa nyakati tofauti, lakini wote walisitishwa kazi Sepemba 19, 2017.
Waandishi hao waliajiriwa na kampuni ya Quality Group lakini mikataba yao ilisitishwa kwa barua kutoka kampuni ya Quality Media Limited na aliyesaini barua za kusitisha mikataba hiyo ni Yusuf Manji mwenyewe.
Miongoni mwa waandishi hao, wapo waliodai mikataba yao ya ajira ilichukuliwa na mwajiri, hivyo walilazimika kuwasilisha barua ya kusitishwa kazi na hati ya kupokea mshahara kuthibisha kuajiriwa kwao.
Hukumu hiyo imeeleza kwa kuwa mlalamikiwa hakufuata utaratibu wa haki katika kusitisha mikataba hiyo, waandishi hao wana haki ya kupewa sehemu ya mishahara iliyokuwa imebaki katika mkataba wao wa kazi ambayo jumla yake ni Sh milioni 232.
No comments:
Post a Comment