WILAYA YA MAGHARIBI B
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kutoa fursa na haki kwa Watu wenye Ulemavu na kuhakikisha kunakuwa na maendeleo jumuishi yanayozingatia mahitaji yao.
Ameyasema hayo wakati akimkaribisha Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid kwenye mafunzo ya maendeleo jumuishi kwa wajumbe wa Kamati tatu za Baraza la Wawakilishi ikiwemo Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Ustawi kwenye ukumbi wa mkutano wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa ndege.
Mhe Harusi amesisitiza kuwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu inahakikisha kuwa Watu wenye Ulemavu wanashirikishwa kwenye masuala ya maendeleo ya kiuchumi katika nchi yao kwa kusimamia sheria na sera ya Watu wenye Ulemavu ili lengo la serikali la kutoa haki na fursa liwe linatekelezwa.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe Zubeir Ali Maulid ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kufanya kazi na kuwa karibu na Kamati za Baraza la Wawakili katika kutoa mafunzo yanayohusiana na Watu wenye Ulemavu ili kuwajenga uwelewa na kufahamu fursa zao pamoja na kuzingatia masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Aidha Alhaj Zubeir amewasihi Wajumbe hao wa Kamati kuhakikisha wanazingatia huduma stahiki wanazotakiwa kupatiwana Watu wenye Ulemavu katika jamii inayowazunguka na kuona kila penye fursa kunakuwa na mazingatio kwa Watu wenye Ulemavu.
Mhe Zubeir amesema Kamati za Baraza la Wawakilishi zinanafasi na mchango mkubwa katika kusimamia masuala ya Watu wenye Ulemavu hivyo mafunzo waliyoyapata wanatakiwa kuyazingatia ipasavyo na kufikisha ujumbe kwa wanajamii ili dhamira ya kuwa na maendeleo jumuishi yaweze kufikiwa.
Nae Mkurugenzi wa mradi wa kushughulikia malezi na makuzi ya watoto wadogo Zanzibar Bi Sharifa Suleiman Majid ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aidha amesema kutolewa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Baraza la Wawakilishi ni kuwakumbusha kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu kupata haki zao ipasavyo kama walivyo watu wengine ili wote wawe walimu wazuri kwa jamii inayotuzunguka.
Wakitoa ushuhuda kwenye mafunzo hayo juu ya mtazamo wa wanajamii mwalimu wa skuli ya sekondari Mpendae Bi Yumna Mmanga na Bw Mohammed Salum kutoka Jumuiya ya Watu wasioona ZANAB wameiomba Wajumbe hao kuwaona Watu wenye Ulemavu kwa utu wao na kuwa hukumu kwa hali zao.
“Mtu mwenye Ulemavu anaweza kufanya kitu chochote cha maendeleo katika jamii na serikali ikiwa tu ataekewa mazingira rafiki na wezeshi” alisisitiza Yumna.
Akifunga mafunzo hayo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe Mgeni Hassan Juma ameiahidi Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais kuwa, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wataendelea kusimamia na kutetea kundi maalum la Watu wenye Ulemavu pamoja na kuhakikisha wanafuata mikataba ya kitaifa na kimataifa iweze kutekelezeka.
Pia amewasisitiza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaposaini mikataba yeyote kuhakikisha inawasaidia Watu wenye Ulemavu pamoja na kusimamia Wizara ambazo bado hazijakidhi miundombinu rafiki kwa matumizi ya Watu wenye Ulemavu kuhakikisha wanasimama kidete kutetea maslahi yao.
“Mafunzo tuliyoyapata hapa yanaumuhimu wa kipekee hasa katika kujenga ushirikishwaji kwa kila mtu ambapo Katiba yetu, sheria zetu, mipango yetu ya maendeleo pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi zote zinaelezea kuwa hakuna kuachwa mtu nyuma”.
Akitoa maoni yake Mjumbe wa Kamati ya Ustawi Jamii Mhe Mwantatu Mbarouk amewaomba wajumbe wa Kamati kujitahidi kuzisoma sheria na kuzifahamu, kutoa ushauri na kuwatetea kwa mujibu wa sheria na kwa upande wa waajiri amewakumbusha kuhusu umuhimu wa kuwapa ajira Watu wenye Ulemavu pamoja na kuitaka jamii kutoa ushirikiano.
Mradi wa Mafunzo ya Maendeleo Jumuishi katika Jamii unatekelezwa ndani ya Wilaya 3, mbili Unguja na moja Pemba katika shehia tano na kuendeshwa kwa ushirikiano Ofisi ya Mkamu wa Kwanza wa Rais, Watu wenye Ulemavu, familia zao, na jamii taasisi za serikali na zisizo za kiserikali zinazohusiana na utoaji wa huduma za afya, elimu, mafunzo ya amali, huduma za jamii na nyenginezo.
No comments:
Post a Comment