HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 10, 2022

WAZIRI MASAUNI AKUTANA NA KAMATI YA MFUKO WA ELIMU, MAIMAMU WA MISIKITI, WALIMU WA MADRASA, AGAWA VIFAA VYA MICHEZO


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya mashindano ya kusoma Quran Tukufu jimboni kwake, leo, ambayo yatafanyika hivi karibuni katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akikabidhi vifaa vya mchezo kwa wanamichezo leo, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa mashindano ya kugombea kombe la Masauni na Jazeera jimboni humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 

 

 Na Felix Mwagara, Zanzibar

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Mhandisi Hamad Masauni, leo, amekutana na Kamati ya Mfuko wa Elimu ya Jimbo, Maimamu wa Misikiti pamoja na Walimu wa Madrasa, kwa ajili ya maandalizi ya mashindano makubwa ya kusoma Quran Tukufu, jimboni kwake, Mjini Unguja, Zanzibar.

Mashindano hayo yatakayofanyika hivi karibuni katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu ambapo washindi mbalimbali watapewa zawadi nono ambazo zitakuwa zimepangwa na kamati hiyo ambayo inaongozwa na Mbunge wa Jimbo hilo.

“Lengo la kukutana hapa, tutoe mawazo mazuri ya kuboresha zaidi katika mashindano yetu ya kila mwaka ambayo yanaibua vipaji na kuwezesha kuongeza elimu ya elimu ya dini kwa washiriki,” alisema Masauni.

Aidha, Mhandisi Masauni aligawa vifaa mbalimbali vya michezo kwa viongozi wa michezo pamoja na wanamichezo jimboni humo ikiwa ni maandalizi ya mashindano mengine aliyoyaandaa ya kugombea kombe la Masauni na Jazeera yatakayoanza hivi karibuni jimboni humo.

Msauni alisema mashindano hayo yanazidi kuimarika na yamekuwa makubwa kutokana na maandalizi yake na wao viongozi kuyajali zaidi kwa lengo la kuibua vipaji mbalimbali jimboni humo.

“Kama kawaida tumeandaa zawadi nzuri zaidi kwa washindi, hivyo nahitaji mashindano ya amani, ya furaha, vurugu hazitakiwi na atakayefanya vurugu huyo tutamshughulikia kwa kuwa sio mwenzetu, michezo inaleta amani, umoja na ushirikiano na sio ugomvi kuumizana, tushindane kwa furaha,” alisema Masauni.

Vifaa vya michezo vilivyotolewa na Masauni ni Jezi na mipira kwa timu mbalimbali zitakazoshiriki mashindano hayo, ambapo gharama ya mashindano hayo mpaka yatakapokamilika ni zaidi ya shilingi milioni ishirini.

Kila mwaka mashindano ya Quran Tukufu pamoja na kugombea Kombe la   Masauni na Jazeera uandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo Kikwajuni, Hamad Masauni pamoja na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salum Jazeera, ambapo wanaandaa mashindano hayo kwa lengo la kupata vipaji vya wasomaji Quran, kuibua vipaji vya michezo mbalimbali na kuwaweka pamoja wananchi wa jimbo hilo kupitia mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages