HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 25, 2022

Taasisi ya Wanawake 100,000 yampongeza Rais Samia nyongeza 23.3% misharaha


 Mkurugenzi wa Haki za Wanawake wa Taasisi ya Wanawake 100, Josephine Matiro akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza asilimia 23.3 ya kima cha chini cha mishahara.
 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Taasisi ya Wanawake Laki Moja (100,000) nchini imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza aslimia 23.3 ya kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma.

Aidha, taasisi hiyo imempongeza Rais Samia kwa uzinduzi wa Filamu ya Royal Tour kwani matunda yake yameanza kuonekana ikiwemo watalii kuongezeka kutembelea vivutio vya utalii.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Haki za Wanawake wa Taasisi hiyo, Josephine Matiro amesema kwa takribani miaka 7 kulikuwa hakuna ongezeko hilo na kwamba katika mwaka mmoja wa Rais Samia ameongeza kiwango hicho.

" Ongezeko hili litaongeza mchocheo wa uchumi, kusaidia kupunguza ukali wa maisha, ari na chachu ya wafanyakazi kufanya kwa bidii bila manung'uniko kama ilivyokuwa awali," amesema Josephine.

Amebainisha kuwa katika nchi za jirani ongezeko lao halijafikia ongezeko hili kwani nchi ya Kenya wameongeza kwa asilimia 12 huku Rwanda na Uganda ikiwa chini ya asilimia 10.

Amesisitiza kuwa  ndani ya mwaka mmoja Rais Samia amechukua hatua mbalimbali ikiwemo kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 9 hadi 8, utoaji ajira mpya, upandishaji madaraja watumishi, ulipaji malimbikizo ya mishahara, ulipaji wa mafao ya wastaafu kwa wakati pamoja na kuongeza umri wa ukataji bima ya watoto kutoka miaka 18-23.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi wa taasisi hiyo ambaye pia ni Balozi wa Utalii, Nangasu Warema amesema Rais Samia ameonesha ushupavu na ujasiri kutokana na kutangaza utalii wa nchi kupitia Royal Tour.
Amesema  Tanzania ni miongoni mwa nchi 9 zilizofanya Royal Tour ikiwemo Rwanda, Israel na Mexico hivyo imetangaza vivutio vya utalii ikiwemo kuiambia Dunia Mlima Kilimanjaro upo Tanzania na mila na desturi za nchi.

Ameafafnua kuwa wana mkakati kuzunguka nchi nzima kuunga mkono Royal Tour kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo wakianzia Nyanda za Juu Kusini

Nae, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake 100,000, Vicky Kamata amesema wanawake wanapaswa kujivunia Rais Samia na kuondoa fikra potofu kuwa wao ni tegemezi kwani wajiamini wanaweza kufanya mamba makubwa.

Amesema Rais Samia amefanya jambo kubwa la kutoa ruzuku ya Sh Bilioni 100 ya kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment

Pages