HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 25, 2022

Rais Samia aitaka THDRC kutoa elimu ya Katiba, kutetea wanyonge



Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameutaka Muungano wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu kupitia Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchni (THRDC) kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la Katiba ili waijue kiundani.

 Kauli hiyo ameitoa jijini humo katika Maadhimisho ya Miaka 10 ya  THRDC  huku akibainisha kuwa endapo wananchi wataijua kiundani katiba ya nchi  itasaidia kuepusha migongano katika jamii kwani katiba pia imeelezea haki kama msingi wa maisha ya mwanadamu.

Amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na mashirika ya haki za binadamu huku akiwakumbusha watetezi hao kutetea haki za wanyonge wakiwemo watoto wadogo wanaobakwa na kukosa wa kuwatetea kuliko kuegemea kwa wanasiasa  na wanaharakati jambo ambalo Serikali haitakubaliana nalo.

"kama sheria hazipo vizuri semeni,lakini msiseme kwa mapambano,semeni kwa lugha nzuri,mkisema kwa lugha mbaya mtamkasirisha mtu kama mlivyokuwa mnafanya zamani,siwezi kuzuia harakati ila harakati zikiwa changa zina faida zaidi"amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa kazi ya kulinda na kutetea haki za binadamu ni jukumu la watu wote kwa sababu hata maendeleo katika jamii huja kwa kuwepo na haki ndani ya jamii hiyo na ndiyo maana serikali ilizindua Azimio la Arusha mwaka 1967 lililozingatia pia haki za mwanadamu kama msingi wa maendeleo kikatiba.

Rais Samia amefafanua kuwa serikali anayoiongoza itaendelea kushirikiana na mashirika ya haki za binadamu na kuyataka mashirika hayo kuweka wazi baadhi ya mambo yake ikiwemo matumizi na mapato yanayotoka kwa wahisani kama sehemu ya kuendesha shughuli zao.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo,Onesmo Olengurumwa amesema mtandao huo umezindua ripoti yake ambayo inaelezea yale waliyoyafanya ndani ya kipindi cha miaka 10 na yale ambayo wanatarajia kuyafanya siku zijazo huku akiipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuonyesha mwanga na ushirikiano thabiti kwa mashirika ya watetezi wa haki za binadamu.
 
Ameishauri serikali kupitia sera na kuwatambua zaidi ambapo amesisitiza Kuwa wao si wapinzani wa serikali kama inavyodhaniwa na baadhi ya viongozi

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ulianzishwa mnamo mwaka 2012 ambapo kwa mwaka huu wanasherekea miaka 10 tangu mtandao huo kuanzishwa kwake Mwongo mmoja uliopita.

No comments:

Post a Comment

Pages