Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, akizungumza wakati wa kilele cha maonesho ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) jijini Dodoma.
Na WyEST, DODOMA
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Adolf Mkenda (Mb) amevitaka vyuo
na taasisi za mafunzo kuona namna ya kuboresha ufundishaji ili vijana wa
Kitanzania wawe mahiri kwenye fani wanazosomea.
Ameyasema
hayo leo Juni 13, 2022 Jijini Dodoma wakati wa kilele cha maonesho ya
elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (TVET) na kuongeza kuwa ni
muhimu taasisi na wadau wakashirikiana katika utoaji wa mafunzo hayo.
Amewataka
waajiri na wadau wote nchini kuwa karibu na vyuo vya mafunzo ikiwa ni
pamoja na kuvijengea uwezo ili viandae wahitimu wanaohitajika katika
soko la ajira.
"Changamoto
moja kubwa wanayopata wenye vyuo na wanafunzi ni sehemu za kujifunzia
kwa vitendo kwani baadhi ya waajiri wamekuwa wakikataa kuwapokea vijana
hawa. Kumbukeni kuwa hawa ndio waajiriwa wenu wa kesho hivyo mnao wajibu
wa kuwapatia nafasi za mafunzo kwa vitendo," amefafanua Waziri Mkenda.
Aidha,
Mhe. Mkenda amesema ni muhimu sana kwa mitaala inayotumika kufundishia
ikalenga kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii ya Watanzania.
"Wito
wangu kwa wamiliki wa vyuo nchini ni kuhakikisha kuwa wanatoa elimu
bora na sio bora elimu. Pia NACTVET kuhakikisha vyuo vyote vinazingatia
taratibu za uendeshaji na utoaji mafunzo," amefafanua Prof. Mkenda.
Naye
Naibu Waziri, Mhe. Omari Kipanga (Mb) amesema awali Baraza la Taifa la
Elimu ya Ufundi kabla haijaungana na Mamlaka ya Ufundi Stadi lilikuwa na
vyuo zaidi ya 400, lilipoungana na kuunda NACTVET limekuwa na vyuo
zaidi ya 1,200 inavyoviratibu.
"Kwaiyo
matumaini makubwa ya Watanzania yapo NACTVET hivyo tuhakikishe
tunaratibu na kusimamia vizuri. Tukio la leo linatutengenezea picha au
ramani ya wapi tunapotaka kwenda," amesema Mhe. Kipanga.
Kwa
upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma za Maendeleo ya Jamii, Salome Makamba (Mb) amesema wanatambua
kwamba Elimu ya kati ndiyo inayochangia sana katika ajira kwenye
viwanda, maofisi na maeneo mengine mbalimbali.
"Sisi
kama wabunge tutaendelea kuwa pamoja nanyi katika juhudi hizi, tunaomba
muendelee kupeleka maonesho haya ya ubunifu katika ngazi ya Wilaya na
Mikoa ili viwanda, wabunifu na vyuo vya kati waje washindane hapa Dodoma
kutoka pande zote za nchi," amesema Mhe. Makamba.
No comments:
Post a Comment